• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Uhuru alihepwa na kuaibishwa na Wazungu aliposhtakiwa Hague, Muthaura afichua

Uhuru alihepwa na kuaibishwa na Wazungu aliposhtakiwa Hague, Muthaura afichua

NA MOSES NYAMORI

RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta aliaibishwa na kuepukwa na Wazungu kama mgonjwa wa ukoma, punde alipotangazwa kuwa kati ya washukiwa sita kwenye barua ya Ocampo.

Aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura, amefichua dhiki alizopitia Bw Kenyatta kwenye kitabu chake, A Moving Horizon, ikiwa ni pamoja na Bw Kenyatta kutengwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.

“Wakati wa mkutano wa kujadili mizozo ya Somalia na Sudan Kusini jijini London, Cameron alikataa kumwalika Rais Kenyatta. Ilibidi Umoja wa Afrika (AU) utishie kususia kikao hicho, ndipo akaalikwa. Hata alipofika London, hakuchangamkiwa inavyostahili kwa kiongozi wa nchi,” anasema Bw Muthaura.

Kitabu hicho chenye kurasa 456 kinaeleza jinsi mataifa ya Ulaya yaliungana kutaka kuzima azma ya Bw Kenyatta na aliyekuwa mgombea mwenza William Ruto kuwania uongozi mwaka 2013.

“Walimtumia aliyekuwa mshauri wa masuala ya Afrika John Carson kuwaonya Wakenya kuwa maamuzi huwa na matokeo. Kwamba maamuzi mabaya yangeleta matokeo mabaya. Hii ilikuwa sehemu ya njama kuhakikisha kuwa Bw Kenyatta na mgombea mwenza William Ruto hawaingii ikulu,” anasema.

Hata wawili hao walipochaguliwa, Bw Muthaura anasema kwenye kitabu chake kuwa, mataifa ya Ulaya yaliendelea kuwatenga.

“Uamuzi wao ulionekana wazi kupitia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza, William Hague na aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Marekani wa masual ya Africa Johnnie Carson. Wawili hao walisema kuwa uhusiano wa kidiplomasia na washukiwa wa ICC ungefanywa tu katika shughuli muhimu,” anasema.

Mbali na kuaibishwa na kutengwa, Bw Muthaura anasema, Rais mstaafu Kenyatta alilengwa na mashahidi wa kesi yake ICC. Kwamba kulikuwa na jaribio la mashahidi wawili kuitisha Sh50 milioni.

“Walidai kuwa na ushahidi hatari dhidi ya Bw Kenyatta uliomhusisha na kundi la Mungiki. Kwanza waliitisha Sh30 milioni kutoka kwa mawakili wa Bw Kenyatta. Walipofeli, wakaunda nyaraka walizodai kuwa ushahidi na kumfuata Bw Kenyatta mwenyewe, mimi (Muthaura) na aliyekuwa Kamishna wa Polisi Meja Jenerali Mohamed Hussein Ali wakitaka Sh50 milioni,” ameandika Bw Muthaura.

Kitabu hicho kinasema afueni kwa Bw Kenyatta na Bw Ruto ilipatikana tu pale mrithi wa Ocampo, Bi Fatou Bensouda alipotamatisah kesi zao.

Mnamo Disemba 2014, Bi Bensouda alieleza mahakama kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi za waili hao.
Hata hivyo, aliacha mwanya wa kuwakamata endapo kutatokea ushahidi mpya.

Bw Muthaura anaeleza kuwa kwa mara ya kwanza tangu wafunguliwe mashtaka, wawili hao walianza kualikwa na viongozi wa Magharibi.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa kinara wa NHIF Richard Kerich akwepa jela

Mademu, hakikisheni mnazaa na wanaume walio na akili,...

T L