• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Gachagua ataka DCI itenge nafasi za kazi kwa wasomi, wataalamu wa fedha

Gachagua ataka DCI itenge nafasi za kazi kwa wasomi, wataalamu wa fedha

NA JURGEN NAMBEKA

NAIBU wa Rais, Rigathi Gachagua, ameitaka Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kuwapa nafasi wataalamu mbalimbali kujiunga nayo, ili kusaidia katika uchunguzi wa makosa na visa mbalimbali vya uhalifu.

Akizungumza jijini Mombasa wakati wa ufunguzi wa Kongamanao la Wahasibu (ICPAK), Bw Gachagua alieleza kuwa maafisa kadhaa husishia kufanya makosa katika uchunguzi kwa sababu ya kutoelewa ipasavyo masuala fulani.

“DCI inafaa ikubali wataalamu wawe katika vikosi vyao. Baadhi ya maafisa hawa wanaochunguza makosa yanayohusu fedha hawaelewi lolote. Sasa ikiwa anapaswa kuandika ripoti katika masuala ambayo yeye mwenyewe haelewi, itawezekanaje?” akauliza Bw Gachagua.

Kulingana naye, alikuwa ametatizwa sana na maafisa wa upelelezi ambao hawakuwa wakielewa masuala ya fedha, akaunti yake ilipofungwa mwaka 2020.

Bw Gachagua anasema wapelelezi hao hawakuelewa jinsi Sh200 milioni zilikuwa zikitumika kuzaa faida kwa kuhamishwahamishwa kutoka kwa akaunti hiyo hadi nyingine kwa ajili ya shughuli za kibiashara.

“Maafisa walitumwa kuchunguza maisha yangu. Nilikuwa nimeweka pesa zangu katika akaunti moja ya kibiashara kwa miaka minane. Faida ya riba nayoipata naihamisha kwenda kwenye akaunti nyingine, inapata faida nairejesha.

Aliyekuwa akinichunguza kwa kutoelewa alisema ninapata Sh800 milioni kila mwaka. Hili halingefanyika kama kungekuwa na mhasibu katika kikosi,” akasema Naibu wa Rais.

Aliwashauri wahasibu kutuma maombi ya kuwa maafisa makadeti kusaidia vikosi vya ulinzi kufanya uchunguzi wa makosa ya kifedha.

 

  • Tags

You can share this post!

Baraza la Magavana Nchini lamruka Gachagua kuhusu mgano wa...

Mameneja wa kampuni ya Wildlife Works wamwaga unga kwa...

T L