• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 6:55 AM
Gachagua atetea ziara nyingi za nje ya nchi anazofanya Rais Ruto

Gachagua atetea ziara nyingi za nje ya nchi anazofanya Rais Ruto

NA FARHIYA HUSSEIN

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametetea vikali safari nyingi za nje za Rais William Ruto akisema zinatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

Gachagua alisisitiza kuwa ziara hizi za kidiplomasia zinaleta manufaa dhahiri kwa taifa akibainisha kufaidi kwa sekta ya utalii.

Naibu Rais alitaja ongezeko kubwa la wageni katika hoteli za pwani kama mfano bora na uthibitisho wa faida za kiuchumi zinazoletwa na ziara za Ruto nje ya nchi.

“Msimu wa likizo unakaribia, ukweli ni kwamba hoteli tayari zimejaa na hii ni kutokana na juhudi za safari za nje za Rais katika kuitangaza Kenya kama pahala pazuri pa watalii, hatimaye kukuza ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa nafasi za kazi,” alisema Bw Gachagua.

Naibu Rais alibaini hali hiyo imewalazimu Mawaziri ambao kwa sasa wako Mombasa kutafuta njia nyingine ya malazi baada ya hoteli mbalimbali kuwafahamisha kuwa wamejaa kwa ajili ya msimu wa sikukuu.

Mawaziri wanatarajiwa kuwa na kikao leo Ijumaa na Rais Ruto katika Ikulu ya Mombasa.

Kiongozi wa nchi alianza ziara yake ya siku tano katika eneo la pwani siku ya Jumanne.

Mfalme Charles III na Malkia Camilla pia wako Mombasa ambapo leo Ijumaa wanatarajiwa kuzuru maeneo mbalimbali yakiwemo Fort Jesus, na Msikiti wa Mandhry eneo la Old Town.

“Watu wanahukumu safari za nje bila kuelewa faida ambazo zimeathiri nchi. Kenya sasa inajulikana duniani kote kutokana na safari za Rais Ruto nje ya nchi, ameitangaza nchi yetu vizuri sana na tumeanza kuhisi matokeo yake kiuchumi,” alisema Bw Gachagua ambaye hivi majuzi alikuwa Ujerumani kwa safari ya kikazi.

Wiki iliyopita Rais Ruto alitetea ziara zake nyingi nje ya nchi akisema zimeathiri pakubwa na kufungua masoko ya mazao ya humu nchini.

Rais Ruto alitajwa kuwa ndiye aliyefanya idadi kubwa zaidi ya safari za kwenda nchi za nje katika kipindi cha mwaka mmoja, hadi kufikia Oktoba alikuwa amefanya safari 38 katika nchi za nje tangu aingie ofisi kama rais Septemba 2022.

Bw Gachagua alikuwa akizungumza mjini Mombasa ambapo alimtaka Gavana wa Kaunti hiyo Abdulswamad Nassir kufanya kazi kwa karibu na utawala uliopo ili wakazi kupata huduma.

Bw Nassir alichaguliwa kuwa gavana wa Mombasa kupitia chama cha Orange Democratic Party (ODM).

“Bwana Nassir, nilikuwa rafiki sana wa marehemu baba yako. Naomba nikushauri, fanya kazi kwa karibu na Rais, tukiwa hapa wewe ni mtu mzuri na unatusifu lakini dakika tunapoondoka unakuwa mtu wa kimya,” alisema Gachagua.

  • Tags

You can share this post!

Masaibu ya chokoraa wa kike wasiopata huduma za upangaji...

Wakazi wa Murogi waomba serikali ibadilishe jina la mtaa...

T L