• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Masaibu ya chokoraa wa kike wasiopata huduma za upangaji uzazi licha ya dhuluma za kingono

Masaibu ya chokoraa wa kike wasiopata huduma za upangaji uzazi licha ya dhuluma za kingono

NA FRIDAH OKACHI

HOFU ya kudungwa sindano wanayosema huenda ikawa na sumu, imefanya chokoraa wa kike kuwa wazazi wakiwa wangali wadogo kiumri.

Ni sikitiko kwamba wengi hata kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 ya kuingia utu uzima, huwa tayari wamejifungua watoto ama wawili au zaidi.

Watoto hao ambao hawajabahatika kupata elimu mjini Eldoret, wengi wao wamepata watoto zaidi ya watatu.

Kuna msichana wa umri wa miaka 14 ambaye ni miongoni mwa watoto 46,639 wanaoishi kwenye mtaa, akiwa na watoto watatu na anaepuka kutumia mbinu ya upangaji uzazi, akihofia huenda akauawa.

“Nina watoto watatu kwa sababu ukweli usemwe, sikuweza kuwaepuka hawa vijana wa kiume miongoni mwetu. Kila wakati tulilala pamoja… wanakulazimisha na hawawezi kukusikiliza,” anasimulia msichana huyo.

Pia anaeleza kwamba kando na hofu, unyanyapaa hufanya wajione duni wakitafuta matibabu hospitalini.

“Hizo hospitali mimi siziamini. Madaktari na wauguzi hawapendi sisi mashefa,” anasimulia akimaanisha chokoraa.

“Nilizaliwa kwa ushefa na sikupenda kuishi hapa. Mama na baba walikuwa ‘mashefa’. Sijui ni nini kilimuua mama? Niliachwa na ndugu zangu watano. Hapa mtaani nimepigwa, nikadhulumiwa kingono na sasa nina watoto watatu. Aki Mungu tu Anisaidie,” anafunguka.

Naye msichana mwingine mwenye umri wa miaka 16, tayari ni mama wa watoto wanne.

“Nilitoka Kitengela nilikokuwa ninakaa na mama wa kambo. Nilipanda malori yakanifikisha hadi mjini Eldoret. Hapa nilikutana na ‘mshefa’ aliyenielekeza,” anasimulia msichana huyu wa pili.

Shirika lisilokuwa la serikali liitwalo Academic Model Providing Access to Healthcare (AMPATH) liko mstari wa mbele kuangazia masaibu ya wasichana hawa. Dkt Sylvester Kimaiyo anasema baadhi ya watoto huripoti kwenye kituo hicho kupata usaidizi wa matibabu.

“Tunapokea zaidi ya watoto 64 wa kurandaranda mtaani kila siku, walioathirika na virusi vya Ukimwi pamoja na wale wa kupokea sindano ya kupanga uzazi. Lakini wengi wao wakihofia kujia matibabu kwa sababu ya kuhisi wenyewe kwamba wananyanyapaliwa,” anaeleza Dkt Kimaiyo.

Dkt Kimaiyo anasema kufanya kazi hiyo na watoto walio na umri mdogo ina umuhimu wake.

“Ni vizuri kufanya kazi na watoto kwa sababu unapowaonyesha ule karibu, wanafunguka na kueleza yale wanayopitia na inakuwa rahisi kujua jinsi ya kuwasaidia isipokuwa wanadhulumiwa na wengi wao wananyamaza na huwezi kujua kwa haraka,” anaeleza.

Aidha anaelezea changamoto anayokumbana nayo kutokana na kufanya kazi na watoto wenye umri mdogo, ni kukosa uelewa wa masuala mengi ya upangaji uzazi.

Dkt Kimaiyo ameelezea Taifa Leo, wengi wa watoto hao hawana elimu kuhusiana na umuhimu wa upangaji uzazi. Hali hiyo imefanya wengi wao kukataa kudungwa wakisema huenda ni dawa ya kuwaua.

  • Tags

You can share this post!

Mahasla wafunga biashara kupisha Mfalme Charles III kuingia...

Gachagua atetea ziara nyingi za nje ya nchi anazofanya Rais...

T L