• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Ichung’wa: Uhuru anasumbua, hatishiwi na serikali

Ichung’wa: Uhuru anasumbua, hatishiwi na serikali

Na WANGU KANURI

KIONGOZI wa wengi bungeni Kimani Ichung’wa amekanusha madai kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anatishiwa na serikali ya Rais William Ruto.

Kwenye ujumbe wake, Ichung’wa alisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza inamheshimu sana Bw Kenyatta lakini anapaswa kuheshimu serikali inayoongoza kwa sasa.

Mbunge huyo wa Kikuyu, hali kadhalika alidai kuwa anachohofia Bw Kenyatta ni kutofanikiwa kwa maandamano yaliyokuwa yakifanyika.

“Kile kinachomuwasha Bw Kenyatta ni kufeli kwa maandamano aliyokuwa akifadhili ili kutishia serikali ili aweze kuyalinda mali yake ambayo aliyapata kwa njia isiyofaa,” akasema.

Aliongezea, “Hakuna anayekutishia kwani una haki kama rais mstaafu. Katiba ya nchi hii inakulinda na hakuna atakayekuhujumu. Wakenya wanataka tu mazingira mema ambayo wataweza kuendeleza na kukuza biashara zao ambazo wewe na Raila Odinga mliharibu kupitia handsheki.”

Ichung’wa pia alilia uharibifu wa uchumi huku akimrai Bw Kenyatta kuipa serikali ya Rais Ruto muda kurekebisha uovu waliofanya.

Katika mkutano maalumu wa kitaifa wa Wajumbe (NDC) uliofanyika Jumatatu, Mei 22, 2023, kinara wa upinzani Bw Odinga alimshukuru Bw Kenyatta kwa kusimama imara na kuhepa vitisho vyote vilivyoelekezewa chama chake cha Jubilee.

Mgogoro unaoshuhudiwa kwenye chama hicho unazingira uongozi na umejitawanya kwa makundi mawili.

Kundi moja linaongozwa na Jeremiah Kioni anayeungwa mkono na Bw Kenyatta na lingine linaongozwa na mbunge maalum Sabina Chege na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Kanini Kega.

  • Tags

You can share this post!

Mkurugenzi wa Kebs mashakani kwa wizi wa sukari hatari

Idadi ya waliofariki Shakahola yasalia 240 upasuaji maiti...

T L