• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Jinsi wanawake warembo wanavyotumiwa kuwapora madereva wa trela usiku

Jinsi wanawake warembo wanavyotumiwa kuwapora madereva wa trela usiku

Na LUCY MKANYIKA

KUNDI la wanawake limekuwa likitumiwa kama chambo kuwahadaa madereva wa matrela wanaosafiri usiku kwenye Barabara Kuu ya Northen Corridor, Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI) imefichua.

Maafisa wa DCI wanaochunguza visa vya ukosefu wa usalama vya hivi majuzi wamebainisha kuwa kundi la visura watano limekuwa likiwalenga madereva kwenye mkondo wa Mackinnon-Mtito Andei, Kaunti ya Taita Taveta.

Haya yanajiri huku visa vya ukosefu wa usalama vikikithiri kwenye barabara hiyo inayoanzia Mombasa na hadi Malaba, ikiunganisha Bandari ya Mombasa na mataifa mengine Afrika Mashariki.

Wasafirishaji mizigo kutoka Kenya, Demokrasia ya Congo, Burundi, Rwanda, Uganda na Afrika Kusini wamelalamika kuhusu ukosefu wa usalama kwenye barabara hiyo hali ambayo imesababisha hasara ya mabilioni ya fedha.

Katika kisa cha hivi majuzi mwezi Novemba, dereva mmoja alipatikana akiwa ameaga dunia ndani ya trela katika eneo la Maungu.

Washambulizi wake walichota mafuta kwenye trela yake kabla ya kutoweka na kufikia sasa hakuna yeyote aliyekamatwa.

Mkurugenzi wa DCI, mjini Voi, Raria Muriuki, amesema mashahidi waliohojiwa na wapelelezi walidai kuwa wanawake warembo katika ujana wao hutumiwa kuwalaghai madereva wa matrela hasusan nyakati za usiku.

Alisema wanawake hao hujifanya wateja kabla ya kuwaelekeza madereva hao kwenye mitego yao.

Baadhi ya madereva ni wahasiriwa wa kundi hilo huku wengine wakiishia kufariki na baadhi kunusurika wakiwa na majeraha.

Alifichua kuwa visa vingi vya wizi vilivyoripotiwa na madereva wa matrela vinahusu wanawake ambao wanafuatiliwa na wapelelezi.

“Inaaminika wanawake hao wanafanya kazi kama genge na kuwalenga madereva kwa kuomba lifti. Hata hivyo, bado hatujawakamata kwa sababu hakuna ambaye ameweza kutuelezea bayana kuhusu wanawake hao,” alisema.

Takwimu kutoka Muungano wa Madereva wa Matrela wa Masafa Marefu nchini zinaashiria kuwa madereva wawili wameshambuliwa na kuuawa na majambazi huku visa vinane vya wizi wa magari vikiripotiwa mwaka huu 2021 kwenye mkondo wa Mackinnon-Mtito Andei.

Mwenyekiti wa Muungano huo Roman Waema ametaja mkondo huo kama eneo hatari.

Alisema Muungano huo umewasilisha ombi kwa Inspekta Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai ukimtaka kuingilia kati.

  • Tags

You can share this post!

Mke kizimbani kwa madai alimmwagia ‘mpango’ petroli

Shujaa yanyoa Amerika ya kocha Mike Friday bila maji raga...

T L