• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Jumwa aponyoka pingu kesi ya uuaji

Jumwa aponyoka pingu kesi ya uuaji

NA BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, Jumanne aliponea chupuchupu agizo la kukamatwa kuhusiana na kesi ya mauaji inayomwandama.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo inayohusu mauaji ya mfuasi wa ODM, Jola Ngumbao, yaliyotokea mwaka wa 2019, ulikuwa umeomba mahakama iagize Bi Jumwa akamatwe wakati wakili wake alipodai kuwa anaugua, kwa hivyo kesi iahirishwe.

Kesi hiyo ilitarajiwa kusikilizwa kwa siku nne mfululizo wiki hii baada ya kuahirishwa kwa muda mrefu.Kupitia kwa wakili wake, Bw Danstan Omari, mbunge huyo alisema hayuko sawa kiafya hivyo basi hangeweza kusafiri hadi Mombasa kuhudhuria kesi yake.

“Bi Jumwa amekuwa mgonjwa. Ameshauriwa na madaktari wake kupumzika kwa siku tano,” Bw Omari alimwambia Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa, Anne Ong’injo.

Wakili huyo alisema Bi Jumwa yuko tayari kwa kesi yake lakini aliomba kesi hiyo iahirishwe ili kumpa muda apate nafuu.

Hata hivyo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ilipinga ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo na kuyataja madai ya ugonjwa kuwa kisingizio cha kuchelewesha kesi.

Upande wa mashtaka ulipendekeza amri ya kukamatwa kwa mbunge huyo itolewe kwa kukosa kufika kortini.

Jaji aliomba kupewa hati za hospitali zilizotiwa sahihi na kutiwa muhuri ili kuthibitisha kuwa mbunge huyo alikuwa mgonjwa.

Hati hizo zilipotolewa, Jaji aliruhusu kesi iahirishwe lakini akasema ripoti ya kina ya matibabu iwasilishwe mahakamani mwezi ujao wakati kesi hiyo itakaposikizwa.

“Kesi itaendelea Februari 1,” akasema.

Kesi hii imeahirishwa mara kadhaa tangu ilipoanza, licha ya upande wa mashtaka kusema ina mashahidi tayari.

Ilipangwa kusikilizwa kwa mara ya kwanza mnamo Februari 2021, lakini kutoka wakati huo, kesi hiyo imesukumwa mbele mara kadhaa hadi sasa.

Mnamo Julai 2021, mahakama ililazimika kuahirisha kesi hiyo mara mbili baada ya Bi Jumwa kuwaondoa mawakili wote wanne ambao wamekuwa wakimwakilisha pamoja na mshukiwa mwenzake, Bw Geoffrey Otieno Okuto.

Hatua hiyo ililazimu mahakama kumpa Bw Okuto muda wa kutosha kuteua wakili mpya. Hapo awali, mawakili Jared Magolo, Cliff Ombeta, Bw Omari, na Shadrack Wamboi waliwawakilisha wawili hao.

Kesi ilipopangwa kusikizwa kwa siku tatu mfululizo wiki moja baadaye, kesi hiyo ilikosa kuendelea tena kwa sababu Bw Okuto hakuwa amepata wakili wake.

Alipopata wakili, kesi hiyo iliahirishwa tena ili kumwezesha wakili huyo kuifahamu kesi hiyo na kupatiwa ushahidi na taarifa za mashahidi ambazo upande wa mashtaka utategemea.

Wakati uo huo, Bw Okuto pia alihitajika kutafuta mdhamini mpya baada ya kuibuka kuwa kuna mipango ya kutoa mdhamini ambaye alimsimamia tangu wapewe dhamana mwaka wa 2020.

Bi Jumwa na Bw Okuto wameshtakiwa kwa mauaji ya Ngumbao wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda.

Wawili hao wamekana kosa hilo.

Mahakama imefahamishwa kuwa marehemu ambaye alikuwa mjomba wa MCA wa wadi ya Ganda, Bw Reuben Katana, alipigwa risasi wakati Bi Jumwa, Bw Okuto, na wafuasi wao walidaiwa kuvamia nyumba ya Bw Katana na kusababisha fujo.

Upande wa mashtaka umekusanya mashahidi 32 kuthibitisha kesi yake dhidi ya wawili hao.

You can share this post!

Sevilla wamsajili Martial kutoka Man-United kwa mkopo

Urembo wa punda ni kitega uchumi Lamu

T L