• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Ni kweli visa vya uhalifu vimepungua Ruiru, kamanda akariri kauli ya Rais

Ni kweli visa vya uhalifu vimepungua Ruiru, kamanda akariri kauli ya Rais

NA MWANGI MUIRURI

KAMANDA wa polisi wa Ruiru Bw Alexander Shikondi amesema Rais William Ruto hakudanganya mnamo Desemba 17, 2023, alipohojiwa moja kwa moja na runinga za kitaifa na kusema kwamba mradi wa serikali wa ujenzi wa nyumba umepunguza visa vya uhalifu.

“Si mimi ninayedai hivyo bali ni takwimu zinazothibitisha hayo. Visa vya uhalifu vimepungua Ruiru kufuatia ajira kwa vijana katika miradi yetu ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu kutokana na ushuru tunaookota,” Rais Ruto akasema Jumapili akiwa katika Ikulu.

Bw Shikondi amekubaliana na kauli ya Rais akisema kwamba ni ukweli kwamba siku hizi katika mitaa ya Ruiru “tumepata afueni kubwa kwa kuweka vijana hawa wetu katika ajira”.

“Kati ya visa 25 kwa wiki ambavyo vilikuwa vinaripotiwa kwa wiki katika stesheni zilizo ndani ya eneo la shughuli za biashara la Ruiru, vimeshuka hadi idadi hiyo kuwa chini ya visa vitano,” akasema Bw Shikondi.

“Hata ule msukosuko ambao tulikuwa nao kuhusu kuchipuka upya kwa kundi haramu la Mungiki, hatari hiyo imeenda chini kwa asilimia 80,” akasema.

Bw Shikondi alisema kwamba “sisi katika usalama tumeona manufaa halisi ya Rais Ruto katika juhudi zake za kuimarisha usalama kupitia kuwaweka vijana kwa riziki”.

Bw Shikondi aliongeza kwamba “tunakadiria kwamba kabla ya miaka miwili kuisha tutakuwa na mazingara muafaka ambayo yatakuwa yanawapa vijana wengi ambao hushawishika kwa urahisi kuingia katika uhalifu mianya ya kutulia ndani ya sheria wakiboreshewa maisha yao”.

Bw Shikondi alisema vyombo vya usalama kwa sasa vinapiga jeki juhudi za Rais za kuimarisha maisha ya vijana kupitia kuwashawishi wajiunge na taasisi za kiufundi na pia kuwafungia mang’weni ya pombe haramu na mihadarati.

“Tumezindua kampeni kali za kuwahimiza vijana ambao hawana taaluma yoyote wajiunge na taasisi za kiufundi ambazo pia serikali inatoa ufadhili wa juu kwa watakaojiunga nazo. Pia, tumepunguza misako ambayo hutekelezewa vijana ili tupalilie uhusiano mwema ambao utatuwezesha kujadiliana nao kwa manufaa yetu sote,” akasema.

Bw Shikondi aliongeza kuwa polisi wamefurahishwa sana na imani ambayo Rais aliwaonyesha katika kuwatutumia kama mfano wa utawala bora na “hatutamwangusha kamwe”.

  • Tags

You can share this post!

Kidato cha Kwanza: Waziri afichua watahiniwa 28,052...

Mwitaliano apokonya Mkenya Chager ubingwa EA Safari Classic

T L