• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kidato cha Kwanza: Waziri afichua watahiniwa 28,052 walipuuza kuchagua shule

Kidato cha Kwanza: Waziri afichua watahiniwa 28,052 walipuuza kuchagua shule

NA WINNIE ATIENO

WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza wataripoti kwa shule zao kuanzia Januari 15, 2024, baada ya matokeo ya uteuzi kuanikwa rasmi Jumatatu, Desemba 18, 2023.

Wizara ya Elimu imekamilisha mchakato wa kuwapa nafasi kwa shule za umma takriban watahiniwa 1.4 milioni wa Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE 2023) kuendana na sera ya kuhakikisha asilimia 100 ya kujiunga na Kidata cha Kwanza.

Hata hivyo si wote waliopata alama 400 kwa KCPE 2023 wamejiunga na shule za kitaifa kwa sababu walikosa kuchagua mapema shule anbazo wangependelea kujiunga nazo. Sasa watahiniwa hao watapewa nafasi katika shule za umma za upili za kiwango cha kaunti ndogo.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amesema jumla ya watahiniwa 28,052 hawakuchagua shule yoyote katika kategoria mbalimbali zinazotambulika. Kati ya hao, 222 wangejiunga na shule za kitaifa nao 4,837 wangejiunga na shule za kiwango cha mkoa.

Wengine 8,716 wangejiunga na shule za kiwango cha kaunti nao 14,277 walikuwa wa kujiunga na shule za kaunti ndogo kwa mujibu wa matokeo yao ya KCPE.

“Inasikitisha kwamba baadhi ya watahiniwa hawakuchagua shule yoyote na idadi yao ni 28,052,” akasema waziri Machogu.

Bw Machogu ameongeza: “Suala hili lilifanya tutafakari ambapo maafisa wa elimu walifikia uamuzi kwamba watahiniwa hao wapate nafasi katika shule za sekondari za kiwango cha eneobunge au kaunti ndogo na ambazo ziko karibu na shule za msingi ambako walisomea.”

Data kutoka kwa wizara zinaonyesha wanafunzi 62,007 wamepata nafasi katika shule zilizo nje ya kaunti zao za kufanyia mtihani wa KCPE.

Idadi ya watahiniwa mwaka 2023 ilikuwa ya juu ambapo kulikuwa na 180,000 zaidi ikilinganishwa na mwaka 2022.

Idadi kubwa ya waliopata nafasi nje ya kaunti zao za kufanyia mtihani ni wale wa Nairobi (27,995), wakifuatiwa na wale wa Kwale (9,185), Narok (8,236) na Kilifi (7,800).

Wengine walikuwa ni wa kutoka Mombasa (4,662), Kajiado (3,396) na Isiolo (733).

“Serikali imejiandaa kuongeza nafasi Nairobi, ambapo imeanza kujenga madarasa 3,500 ,” amesema.

Aidha, shule zilizokuwa na idadi kubwa ya watahiniwa zilikuwa ni Kabianga (wavulana) na Pangani ya Nairobi (wasichana)

Waziri amewataka wadau walete rasilimali kuhakikisha mchakato wa kuzindua Sekondari ya Juu mnamo Januari 2026. unafanikiwa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mzee aomba wahisani wampe sehemu ya kuuzika mwili wa mkewe

Ni kweli visa vya uhalifu vimepungua Ruiru, kamanda akariri...

T L