• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Kenya Kwanza inaua ujirani mwema, adai Raila

Kenya Kwanza inaua ujirani mwema, adai Raila

NA LABAAN SHABAAN

KIONGOZI wa upinzani Raila Odinga amelaumu Rais William Ruto akidai uhusiano wa Kenya na mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), umedorora sababu ya utepetevu wa kidiplomasia.

Akirejelea matukio wakati wa sherehe za Jamhuri Dei mnamo Desemba 12, 2023, Bw Odinga alisema kukosa kwa wawakilishi wa EAC katika maadhimisho hayo kuliashiria uhusiano bora wa muda mrefu umeharibika zaidi.

“Wakenya waligundua kuwa kuna shida sana ya uhusiano wetu na majirani wetu wa Afrika Mashariki tulipoadhimisha miaka 60 tangu tupate uhuru,” Bw Odinga alisema kupitia barua kwa vyombo vya habari iliyotumwa Desemba 19, 2023.

 “Hakuna nchi ya Afrika Mashariki iliyowakilishwa katika viwango vya Rais, Makamu Rais ama Waziri Mkuu kama ilivyotarajiwa kuwa desturi katika sherehe hizi muhimu hadi ikachukuliwa vivi hivi tu,” aliongeza.

Hata hivyo, Rais Ruto alipinga madai kuwa tukio la Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu kutohudhuria sherehe hizo ni ishara ya kutibuka kwa uhusiano wa mataifa haya.

“Kwani mimi huhudhuria sherehe za kitaifa za mataifa mengine? Hapana, ina maana kuna shida? Hapana,” alifoka Rais akijibu maswali ya wanahabari katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumapili, Desemba 17, 2023.

Akiendeleza msururu wa shutuma kwa serikali ya Kenya Kwanza, Bw Odinga alisema serikali iliyoko madarakani imeanguka mtihani wa masuala ya kidiplomasia akidokeza serikali imelazimisha Uganda kulipia ‘ada ya ubroka’ kwa kutumia barabara ya Kenya kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Mombasa.

“Uganda imelazimika kuenda mahakamani kutafuta afueni ili kujilinda kutokana na uroho wa utawala wa Rais Ruto,” Bw Raila alisema akiongeza imebidi nchi hiyo itafute njia mbadala kupitia Tanzania kusafirisha bidhaa za petroli.

Kadhalika, Kiongozi wa Azimio alikashifu Waziri wa Barabara na Usafiri Kipchumba Murkomen kwa kusema Rwanda ni nchi inayoongozwa kidikteta.

Bw Odinga alisema kauli ya waziri Murkomen ilikosa lugha ya kidiplomasia huku akiomba msamaha kwa raia wa Rwanda sababu ya tukio hilo.

Katika mahojiano ya runinga mnamo Jumatatu, Desemba 18, 2023, Bw Murkomen alisema, “Rwanda si kama Kenya. Rwanda ni taifa linaloongozwa kidikteta ambapo agizo la Rais huwa sheria.”

  • Tags

You can share this post!

Tanzia: Mamake spika wa zamani wa Kiambu aaga dunia

David Mugonyi ateuliwa Mkurugenzi Mkuu wa CA kujaza nafasi...

T L