• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
David Mugonyi ateuliwa Mkurugenzi Mkuu wa CA kujaza nafasi ya Chiloba

David Mugonyi ateuliwa Mkurugenzi Mkuu wa CA kujaza nafasi ya Chiloba

NA LABAAN SHABAAN

WAZIRI wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Uchumi Dijitali Eliud Owalo amemteua Mkuu wa Huduma za Mawasiliano Kirais, Bw David Mugonyi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA).

Akimwandikia barua Mwenyekiti wa Bodi ya CA Bi Mary Wambui, Bw Owalo amemwelekeza kufanya rasmi agizo hilo ili Bw Mugonyi kuanza kazi.

“Nimerejelea barua kutoka kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei ya Desemba 19, 2023 iliyoelekeza kuidhinishwa kwa Bw David Mugonyi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya,” akasema waziri Owalo.

“Unaweza kuendelea kufanya rasmi uteuzi huu,” akaongeza Bw Owalo katika barua aliyoandika na kutuma Desemba 20, 2023.

Kabla ya tangazo hili, Mkuu wa Utumishi wa Umma alimwandikia Bw Owalo barua ya kufanya rasmi nafasi mpya ya Bw Mugonyi.

Bw Koskei alisema Halmashauri ya Wakurugenzi wa CA iliandaa mahojiano ya kazi ambapo Bw Mugonyi aliibuka kidedea.

Bw Mugonyi atahudumu wadhifa huu baada ya Bw Chiloba kujiuzulu Oktoba 19, 2023, bada ya kuandamwa na tuhuma za ufisadi na usimamizi mbaya wa ofisi.

Soma Pia: Ezra Chiloba ajiuzulu kutoka wadhifa wake wa Mkurugenzi Mkuu wa CA baada ya kukabiliwa na tuhuma za ufisadi

Kulingana na ripoti ya ukaguzi, Chiloba alijipendelea kwa kutuma maombi na kuidhinisha mkopo wake wa nyumba kwa kiwango cha juu kwa thuluthi mbili.

Aidha, alidaiwa kujihusisha na mgongano wa kimasilahi kwa kujitwika wajibu wa kuwa mnunuzi na muuzaji katika biashara ambapo CA ililipa Sh25 milioni.

Bw Mugonyi, anayerithi mikoba ya Bw Chiloba, amekuwa akifanya kazi na Rais William Ruto tangu 2013 alipokuwa msemaji na katibu wa mawasiliano wakati Rais alihudumu wadhifa wa Naibu Rais.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Kwanza inaua ujirani mwema, adai Raila

Mkurugenzi wa kampuni ya ukopeshaji pesa Kilifi ashtakiwa...

T L