• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Magari ya kifahari yatumika kusafirisha dawa za kulevya

Magari ya kifahari yatumika kusafirisha dawa za kulevya

NA FARHIYA HUSSEIN

UCHUNGUZI wa Idara ya Upelelezi (DCI) umebaini kuwa baadhi ya magari ya kifahari yanatumika kusafirisha dawa za kulevya.

Katika tukio la hivi punde gari aina ya Toyota Harrier, lilinaswa wakati wa oparesheni ya kusaka dawa za kulevya mnamo Jumatano, ambapo watu wawili walinaswa wakiwa na kilo 477 za bangi, yenye thamani ya takriban Sh14 milioni, kwenye barabara kuu ya Mombasa-Malindi.

Wawili hao, Mabw George Nitti, 37 na Raphael Mbithi, 37, walikamatwa katika eneo la Swallows, Kilifi Kusini kufuatia oparesheni iliyotekelezwa na maafisa wa polisi wanaohudumu chini ya DCI.

Oparesheni hiyo ilisababisha kutwaliwa kwa gari aina ya Toyota Harrier, lililosajiliwa nambari KDK 020B, lililokuwa likitumika kusafirisha dawa hizo haramu.

Kulingana na ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Ndonya, eneobunge la Kilifi Kusini, dereva aligoma kusimamisha, na kuwalazimu maafisa kufyatua risasi kwenye tairi la kulia.

Dawa zilizonaswa na ambazo zilichunguzwa na mwanakemia wa serikali Mombasa, zilifikia kilo 477 zikikisiwa kuwa na thamani Sh14 milioni.

Hii sio mara ya kwanza kwa magari ya kifahari kuonekana yakitumika kusafirisha dawa za kulevya.

Septemba 4, 2023, oparesheni nyingine ya DCI ilinasa gari jeusi aina ya Prado TX lililokuwa likitumiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Katika tukio hilo, kilo 316 za bangi zilizokadiriwa kuwa na thamani ya Sh9 milioni, zilipatikana baada ya gari hilo kupata ajali na kutua kwenye mtaro.

Wakati wa uchunguzi, wapelelezi walipata nambari nyingi za usajili, zinazofanana na zile zinazoonekana kwenye magari ya umma, jambo ambalo lilizua shaka zaidi.

Huku barabara kuu ya Mombasa-Malindi ikionekana kuwa sugu katika usafirishaji wa dawa hizo haramu, mamlaka imeweka wazi msimamo wao kuhusu vita dhidi ya utumizi wa dawa za kulevya katika eneo la Pwani na nchini kwa jumla.

Mwaka jana, 2022, Rais William Ruto, alitangaza vita dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya na wauzaji mihadarati, akihakikishia umma kwamba utawala wake utakabiliana na tatizo la dawa za kulevya katika eneo la Pwani.

Aliwaonya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kuondoka nchini Kenya kabla ya sheria kuwafikia.

“Nimetoa agizo kwamba wote wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya waondoke humu nchini. Wanafaa kwenda kutafuta mahali pengine pa kufanya hivyo,” Rais Ruto alionya.

Rais pia alitoa wito wa kufungwa kwa mianya na njia zote zinazoshukiwa kutumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

 

  • Tags

You can share this post!

Akothee ajipongeza kwa kupata digrii licha ya kusoma kwa...

Nyota wa West Ham Jarrod Bowen machozi tu mpenziwe Dani...

T L