• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Mumias: Mahakama yakubali kujumuisha walalamishi zaidi

Mumias: Mahakama yakubali kujumuisha walalamishi zaidi

RICHARD MUNGUTI NA ELIZABETH OJINA

MAHAKAMA Kuu jana Jumanne iliwajumuisha walalamishi zaidi ya 20 katika kesi ya kupinga kampuni moja ya Uganda kufufua kiwanda cha Sukari cha Mumias, chenye madeni ya Sh30 bilioni.

Wakili James Orengo alikuwa amepinga walalamishi hao kuruhusiwa kushiriki katika kesi akisema “ni watu wasio na mwelekeo.”

Lakini wakili Paul Muite alitofautiana na Bw Orengo pamoja na mawakili wengine waliopinga ombi la walalamishi zaidi kujiunga na kesi hiyo, akisema msimamizi wa kampuni ya Mumias aliyeteuliwa na mahakama, Bw Ponangipali Ramana Rao, kufufua kiwando hicho, hakufuata utaratibu kuteua kampuni ya Sarrai.

Bw Muite alisema kampuni ya West Kenya Limited iliyo na ukwasi mkuu katika sekta ya sukari ilisema itaekeza kitita cha Sh36 bilioni kufufua kampuni.

“Madeni ya Mumias ni Sh30bilioni na West Kenya itaekeza Sh36bilioni kufufua Kampuni ya Mumias katika muda wa miaka 20 na kuwalipa wadeni wote ikiwa ni pamoja na wakulima wa miwa wanaodai mabilioni ya pesa,” alisema Bw Muite.

West Kenya ilisema Sarrai itachukua zaidi ya miaka 80 kufufua kampuni hiyo ikitiliwa maanani haina nguvu kifedha.

Lakini Jaji Wilfrida Okwany, alifahamishwa kuwa tayari kampuni ya Sarrai imeanza kazi ya kukifufua kiwanda hicho.

Wakurugenzi wa Sarrai na wale wa West Kenya ni ndugu wa toka ni toke licha ya kuwa wanahudumu Uganda.

Jaji Okwany alikuwa amesitisha shughuli katika kiwanda hicho hadi kesi iliyowasilishwa na Bw Ochochi na wenzake wanne isikizwe na kuamuliwa.

Jaji huyo alifahamishwa kuwa agizo hilo alilotoa Januari 14 halikufuatwa na Sarrai ilianza kazi mara moja.

Wakulima zaidi ya 10,000 wa zao la miwa kupitia wakili Danstan Omari wanaomba Jaji Okwany aruhusu Sarrai iendelee na kazi kwa vile wakazi wa Magharibi wameathirika mno kwa kutolipwa zaidi ya Sh7bilioni.

Bw Omari alisema kutofufuliwa kwa kiwanda hicho kunaathiri uchumi wa taifa hili. Kesi hiyo itatajwa Machi 14 mwaka huu.

Kwingineko, wafanyikazi katika kiwanda cha miwa cha Chemilil, jana waliandamana baada ya mameneja wawili wakuu waliokuwa wamepewa likizo ya lazima, kurejea kazini.

Shughuli kiwandani humo zilivurugwa karibu siku nzima, huku wafanyikazi hao wakijaribu kuwaondoa Kaimu Meneja Mkurugenzi Gabriel Nyangweso na Meneja wa Fedha, Emmanuel Ngala.

Katibu wa chama cha Wafanyikazi katika Mashamba ya Miwa (KUSPW), tawi la Chemelil, Bw Jack Osida, alisema wafanyikazi wanapinga hatua ya serikali kuwarejesha kazini mameneja hao, kabla uchunguzi kuhusu usimamizi mbaya dhidi yao kukamilika.

“Hatujapata mawasiliano yoyote kutoka kwa wizara ya Kilimo kwa nini mameneja hawa wamerudi kazini kabla ya uchunguzi kukamilika,” akasema Bw Osida.

You can share this post!

Waiguru ataka mgombea mwenza wa Ruto atoke eneo la Mlima...

WIKI YA LUGHA ZA KIAFRIKA: Historia fupi kuhusu chimbuko la...

T L