• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mahindi: Wakulima Bonde la Ufa katika njiapanda

Mahindi: Wakulima Bonde la Ufa katika njiapanda

EVANS JAOLA na BARNABAS BII

WAKULIMA wa mahindi ukanda mwa Bonde la Ufa wanakabiliwa na njiapanda kuhusu kuyauza mahindi yao kwa mawakala wanaotoa pesa za haraka au wasubiri serikali itangaze bei mpya ya kununua mazao hayo.

Mawakala wamefurika katika masoko ambako mahindi huuzwa ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa baada ya wakulima kuyavuna mahindi tele msimu huu.

Kwa sasa wanauza kila gunia la kilo 90 kwa Sh5, 200.

Inakadiriwa idadi ya magunia ambayo yamevunwa sasa yatapanda kutoka magunia milioni 32 msimu uliopita hadi milioni 44 msimu huu. Hii ni kutokana na hatua ya serikali kusambaza mbolea ya bei nafuu na pia hali inayoridhisha ya hewa.

Wakulima wakiendelea kujipata kwenye njiapanda, serikali imewaonya dhidi ya kuyauza mahindi yao kwa bei ya kutupa.

Waziri wa Kilimo Mithika Linturi alisema kuwa serikali ina mpango wa kuyanunua magunia milioni moja ambayo yatapelekwa kwenye Hifadhi ya Chakula Nchini (NFR).

Hifadhi hiyo inatarajiwa kuwa na chakula cha kutosha ili kukwamua nchi wakati ambapo kutakuwa na janga la ukame na njaa. Siku zilizopita, taifa limegubikwa na uhaba wa mahindi na kuilazimu kuyaagiza kutoka nje ya nchi.

“Tunashauriana na Hazina ya Kitaifa ili kuwasilisha pesa za kununua mahindi kutoka kwa wakulima. Tutatangaza bei bora kwa wakulima hivi karibuni,” akasema Bw Linturi.

Waziri huyo alikuwa akizungumza baada ya kukagua vifaa vya kukausha mahindi vya Kampuni ya Mbegu (KSC) mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

Alisema serikali ilikuwa ikilenga kununua mahindi kutoka kwa wakulima kupitia Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao Nchini (NCPB) kwa bei nzuri kwa wakulima.

Bw Linturi alisema wakulima watapata faida tele na kuwataka wawe na subira badala ya kuyauza mahindi yao kwa mawakala ambao wanawahadaa.

Alisema mawakala hao huyauza mahindi hayo kwa bei ya juu wakati wa ukame na kupata faida maradufu.

“Mtandao wa kuwapa wakulima risiti wakiuza mahindi yao sasa unafanya kazi. Kila mkulima yupo hiari kuhifadhi mahindi yake ili kuwazuia kupata hasara zaidi baada ya mavuno,” akasema Linturi.

Wakulima wengi hata hivyo, wanasema heri kuyauza mahindi hayo kwa mawakala badala ya kusubiri bei ya serikali ambayo huwa si ya juu. Pia wanasema gharama ya juu ya kuhifadhi mahindi yao yatawaponza zaidi wasipoyauza kwa sasa.

“Ndege iliyo mkononi ni bora kuliko yule ambayo yupo msituni. Shida pia haijui subira,” akasema Mkulima John Kirui kutoka Chepkumai.

“Matatizo hayajui subira. Wakulima wengi wanataka kulipa karo kwa watoto wao na pia kutimiza mahitaji mengine ya kibinafsi ndiposa wanahiari kuyauza mahindi yao kwa mawakala,” akaongeza.

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ni kati ya viongozi kutoka maeneo ambayo yanakuza mahindi ambao wamewaonya wakulima dhidi ya kuyauza mahindi yao kwa mawakala.

“Lazima tuweke mikakati ya kuzuia mawakala kuwafilisi wakulima wetu. Nawashauri watumie vifaa vya NCPB vya kukausha mahindi kisha wayahifadhi na kuyauza baadaye kwa bei nzuri,” akasema. Bw Natembeya.

 

  • Tags

You can share this post!

Sakaja ataka deni kubwa la NMS lichunguzwe

Vipusa 3 wakamatwa Murang’a wakinengulia walevi viuno...

T L