• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Masoko yaliyogeuka maficho ya wahuni

Masoko yaliyogeuka maficho ya wahuni

NA RICHARD MAOSI

HALI mbaya ya soko katika kituo maarufu cha Kibiashara cha Mlolongo, Machakos imefanya eneo hilo kugeuka maficho ya wahalifu.

Wahalifu wamevunja uzio, kuiba mabati, vyuma vikuukuu na kuuza mbao mitaani.

Vibanda vilivyochanika na barabara zisizoweza kupitika, vimegeuka kuwa mojawapo ya changamoto kwa wafanyibiashara.

Millicent Obonyo mkazi wa barabara ya Katani, anasema yeye ni mfanyibiashara na hulazimika kila siku kufika sokoni mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi (6Am) kuchukua bidhaa.

Hata hivyo, anashauri kuzibwa vichochoro vyote vya kuingia au kutoka sokoni kwa sababu vinatumika kama maficho ya wahalifu wa simu.

Mwaka 2022, aliwahi kuvamiwa na vijana waliokuwa wamejificha katika vibanda vinavyozunguka soko na wakampokonya pesa za mtaji wake.

“Mbali na kurekebisha soko, ingekuwa vyema liwekewe kamera za siri (CCTV) ili iwe rahisi kufuatilia mienendo ya wanaoingia na kutoka sokoni hasa nyakati za usiku,” Millicent akapendekeza.

Hali ni kama hiyo ukizuru soko la Kiamunyeki barabara ya Nakuru-Nairobi, Kaunti ya Nakuru.

Erick Sule ambaye ni mchuuzi wa samaki katika soko hilo, anasema mwanzo anarushia lawama serikali za kaunti ambazo zilianzisha miradi kisha zikakwama.

Anasema hakika hali mbaya ya soko haijawafaidi wale ambao walipaswa kufaidika na miradi yenyewe, kwani serikali za kaunti zimekuwa zikirushiana lawama utawala mpya unaposhika hatamu.

Kulingana na Sule ni kama kila serikali ya kaunti huja na mipangilio yake na wala hawajatilia maanani suala la kurekebisha soko.

Anasema kati ya 2017-2018 soko analohudumu lilistahili kukamilika, ila wenyeji hawakufaidika na mradi wenyewe kwa sababu shughuli zilichelewa.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali anasema Nakuru ni mojawapo ya kaunti nchini ambazo zina idadi kubwa ya vijana ambao hawana ajira.

Baadhi yao hutegemea vibarua vya uchukuzi, kwa kubebea wafanyibiashara mizigo kutoka sokoni ili wajikimu kimaisha.

Licha ya kwamba soko la Kiamunyeki limewekewa uzio, baadhi ya maeneo hutumika kama kituo cha kutupa taka na vijana wanaorandaranda mitaani wamekuwa wakilala humo na kuvamia wapit njia nyakati za usiku.

Aidha, muungano wa wafanyibiashara katika soko la Wakulima Market katikati mwa jiji la Nakuru wangependa kuchimbiwa kisima cha maji ili kuwarahisishia shughuli.

Pia, wangependa kuongezewa walinzi wa usiku ili kuhakikisha bidhaa zao zinabakia salama.

  • Tags

You can share this post!

Amenipachika mimba, ndio, lakini sitaki kabisa kuolewa na...

Mchungaji alia kushindwa kuelekeza wapenzi wanaofarakana,...

T L