• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Mbarak aonya kuhusu uwezekano wa maafisa wa umma kutumia El Nino kama kisingizio cha wizi wa pesa za umma

Mbarak aonya kuhusu uwezekano wa maafisa wa umma kutumia El Nino kama kisingizio cha wizi wa pesa za umma

NA CHARLES WASONGA

AFISA Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak ameonya kuhusu njama ya baadhi ya magavana na maafisa katika serikali kuu kupora pesa za umma kwa kizingizio cha kujiandaa kwa mvua kubwa ya El Nino.

Bw Mbarak alifichua kuwa tume hiyo imekusanya habari za kijasusi kwamba baadhi ya maafisa wa umma katika ngazi hizo mbili za serikali wanapania kuiba pesa hizo kupitia kubuniwa kwa kamati za kuandaa mikakati ya kupambana na mvua ya El Nino inayotarajiwa kuanza Oktoba 2023.

“Wakati huu ambapo El Nino inakuja, watu fulani katika serikali za kaunti na serikali ya kitaifa wamebuni mipango ya kukabiliana na madhara ya mvua hiyo. Mipango hiyo ni mizuri lakini tuna habari na fununu kuwa maafisa hao sasa wamepata mwanya wa kula pesa za umma. Usishtuke kwamba hivi karibuni utaanza kushuhudia sakata mbalimbali,” akasema Jumatano usiku alipohojiwa katika kipindi cha JKLive kwenye runinga ya Citizen.

Bw Mbarak alisema kuwa maafisa wafisadi hujaribu kutumia nafasi inayotokana na aina mbalimbali za majanga ili kujitajirisha bila kuzingatia matokeo yake kwa umma.

“Hii ndio maana Wakenya wasishangae watakapoanza kushuhudia ufisadi kupitia uporaji wa pesa za umma kuanzia mwezi Oktoba mvua ya El Nino itakapoanza,” akasema.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imeonya kuhusu uwezekano wa kushuhidiwa kwa mvua ya El Nino kote nchini kuanzia Oktoba 2023 hadi Januari 2024.

Kufuatia tangazo hilo, Serikali ya Kitaifa imetangaza kuwa itahitaji zaidi ya Sh33 bilioni kutekeleza mikakati ya kukabiliana na madhara ya mvua hiyo.

Nazo serikali kadha za kaunti zimeweka mipango ya kukabiliana na athari za mvua hiyo kubwa.

Kwa mfano, juzi Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alizindua mipango kama hiyo katika uwanja wa Uhuru Park iliyojumuisha kuwaajiri jumla ya vijana 3,500 watakaozibua mitaro ya kupitisha maji katikati na viungani mwa jiji.

Wakati huo huo, Bw Mbarak amekariri kuwa tume yake inawachunguza jumla ya magavana 21 wa sasa na wa zamani kuhusiana na tuhuma mbalimbali za ufisadi.

Hata hivyo, alisema utendakazi wa tume yake unarudishwa nyuma na changamoto kama vile  uhaba wa fedha na idadi ndogo ya wafanyakazi.

  • Tags

You can share this post!

Mchango: Familia ya mtandaoni yampa mtangazaji Kimani...

El Nino: Wanaoishi mtoni kuhamishwa ‘cha lazima’

T L