• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mbunge wa Mukurweini ataka tohara iwe lazima kwa wanaume wote Kenya

Mbunge wa Mukurweini ataka tohara iwe lazima kwa wanaume wote Kenya

Na SAMWEL OWINO

MSWADA unatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa ili kufanya upashaji tohara wanaume kuwa lazima ukitekelezwa na wahudumu wa matibabu.

Mbunge wa Mukurweini John Kaguchia amewasilisha Mswada wa Upashaji Tohara 2023 akisema kupitishwa kwake kuwa sheria kutachangia kupungua kwa magonjwa ya zinaa nchini (STDs).

“Kuruhusu mswada wa upashaji tohara kufanyiwa uangalizi na mtaalamu wa matibabu kunalenga watoto baada ya kuzaliwa na wakifikisha miaka 18. Mswada huu utachangia afya njema na salama,” akasema Bw Kaguchia.

Mswada huo unalenga kupiga marufuku tohara za kitamaduni ambazo huendelezwa na ngariba na sasa shughuli hiyo ya kuingia utu uzima itakuwa ikifanyika hospitalini chini ya mtaalamu wa masuala ya matibabu.

Tohara kwa miaka mingi imekuwa ikichukuliwa kuwa suala la kitamaduni na sasa litakuwa la lazima iwapo mswada huo utapitishwa, japo unatarajiwa kuzua pingamizi tele.

Hata hivyo, Bw Kaguchia anasema kuwa ukataji govi kama sehemu ya tohara utafanyika hospitalini huku mchakato mwingine wa kitamaduni ukiendelea baada ya hapo.

“Hii ni hatua nzuri kwa wavulana kwa kuwa hawatakuwa wakipashwa tohara kwa njia ya kitamaduni ila kupitia mchakato unaoeleweka wa kimatibabu,” akasema Bw Kaguchia.

Kwa mujibu wa mswada huo, baadhi ya watoto wameathiriwa kutokana na upashaji tohara kwa njia ya kitamaduni baada ya uume wao kukatwa vibaya. Hata hivyo, sasa shughuli hiyo itaendeshwa kitaaluma tena mahali ambapo kuna viwango vya juu vya usafi.

“Wataalamu wa kimatibabu watakuwa wakitathmini hali ya kila mtoto na kuangalia afya yake kisha kumfuatilia iwapo tatizo lolote litatokea baada ya kupashwa tohara,” inasema sehemu ya mswada huo.

Bw Kaguchia, ambaye ni mbunge wa UDA, anasema kuwa magonjwa ya zinaa ni hatari kwa afya ya umma na huchangia kupanda kwa gharama ya matibabu na kupotea kwa maisha.

Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukizana (CDC) kimetambua kuwa tohara ya wanaume inapunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa ukimwi kwa kati ya asilimia 50-60.

  • Tags

You can share this post!

Mpango wa kutuma polisi Haiti bado waendelea licha ya korti...

Kesi ya Muingereza anayedaiwa kupiga dafrao na kuua mkewe...

T L