• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 2:11 PM
Kesi ya Muingereza anayedaiwa kupiga dafrao na kuua mkewe Mkenya kuendelea kusikizwa

Kesi ya Muingereza anayedaiwa kupiga dafrao na kuua mkewe Mkenya kuendelea kusikizwa

NA BRIAN OCHARO

RAIA wa Uingereza Simon Harold Shiels, amepata pigo baada ya mahakama ya Malindi kukataa kusitisha shtaka dhidi yake kuhusu kifo cha kutatanisha cha mkewe, Jecinter Njoki.

Jaji Stephen Githinji alitupilia mbali ombi la Muingereza huyo ambapo alitaka shtaka la mauaji dhidi yake litupiliwe mbali na kesi kusitishwa kabisa.

Bi Njoki alifariki Januari 21, 2018, alipogongwa na gari lililokuwa likiendeshwa na mshukiwa huyo kwenye barabara ya Thalathameli-Kaoyeni eneo la Ganda, Kaunti ya Kilifi.

Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa akitoroka kuokoa maisha yake wakati Bw Shiels ambaye alikuwa akiendesha gari lake aina ya Mitsubishi alipogonga na kuiangusha pikipiki iliyokuwa imeabiriwa na Bi Njoki.

Bw Alex Kahindi ndiye aliyekuwa dereva wa bodaboda iliyokuwa imebeba Bi Njoki wakati wa kisa hicho.

Awali, Bw Shiels alikabiliwa na mashtaka ya makosa ya barabarani, lakini baada ya uchunguzi wa miaka mingi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ilirekebisha shtaka hilo na kuliongezea nguvu kuwa la mauaji.

Kosa la trafiki liliondolewa katika mahakama ya Malindi wiki mbili kabla ya shtaka la mauaji kuwasilishwa. Bw Shiels alishtakiwa kwa kusababisha kifo kwa kuendesha gari vibaya.

Bi Njoki na Bw Shiels wanadaiwa kuwa na ugomvi wa nyumbani kabla ya tukio hilo. Inadaiwa kuwa ugomvi huo ulimfanya Bi Njoki kutoroka kuokoa maisha yake.

Ilidaiwa kuwa raia huyo wa uingereza aliwafuata nyuma na kuwagonga na gari lake walipokuwa wakitoroka kwa pikipiki.

Bi Njoki alikufa katika hospitali ya Malindi akipokea matibabu. Ripoti ya upasuaji ilionyesha kuwa marehemu alivuja damu nyingi kutokana na majeraha ya kichwa.

Hati zilizowasilishwa kortini zimefichua kuwa mzozo mkali wa mali ulizuka kati ya Bw Shiels na aliyekuwa mume wa Njoki, Bw Amos Okoth Oluoch, na watoto wake baada ya kifo chake.

Watoto wa mwanamke huyo, Anthony Otieno na Bi Mary Akinyi, pamoja na jamaa zake, walipinga madai ya jamaa huyo kuwa yeye ndiyemrithi pekee wa mali za marehemu.

Katika kesi iliyowasilishwa mwaka wa 2018, Bw Oluoch alimshtaki Bw Shiels kuhusu umiliki wa mali hiyo ambayo ni ya thamani ya mamilioni ya pesa.

Bw Oluoch aliteta katika kesi hiyo kwamba licha ya kutengana kwao, ndoa yao haikuwa imevunjwa rasmi, na kwa hivyo bado alikuwa mume wake halali, kwani walikuwa wameoana chini ya sheria za kitamaduni za Wajaluo mnamo 1981.

“Tulitengana lakini hatukuachana, kwa hivyo mimi bado nina haki ya kufaidika na mahali zake,” alisema.

Hata hivyo, hakutoa ushahidi wa kuunga mkono dai hili la ndoa iliyofanywa chini ya sheria za mila za Wajaluo.

Ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo ulifichua kwamba baada ya Oluoch na Njoki kutengana, mwanamke yuyo aliolewa na Bw Shiels, na wakaishi pamoja kwa miaka michache kabla ya kifo chake 2018.

Karatasi za mahakama pia zinaonyesha kuwa raia huyo wa Uingereza alilipa mahari kwa wazazi wa mwanamke huyo katika ndoa waliofanya chini ya sheria ya kimila ya Gikuyu.

Wakiwa katika ndoa hiyo, wawili hao wanadaiwa kuwa walipata mali huko Malindi yenye thamani ya mamilioni ya pesa.

Hata hivyo, Bw Oluoch alimtaja Bw shiels kama mpenzi wa “kawaida” ambaye alichukua fursa ya kutengana kwao ili kuchumbiana naye.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge wa Mukurweini ataka tohara iwe lazima kwa wanaume...

Mwanawe Rais wa Somalia atoroka Uturuki baada ya kuua...

T L