• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mlinzi auawa katika uvamizi wa Kanisa la PCEA Rironi, wezi waiba ala za muziki na divai

Mlinzi auawa katika uvamizi wa Kanisa la PCEA Rironi, wezi waiba ala za muziki na divai

NA MWANGI MUIRURI

POLISI katika Kaunti ya Kiambu wanawasaka majambazi ambao walivunja Kanika la Kipresibeteria na kuiba zana za muziki na kisha wakakunywa divai.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamanda wa polisi wa Kiambu Bw Michael Muchiri, majambazi hao walivunja Kanisa la PCEA Rironi mwendo wa usiku wa manane na kutekeleza hasara hiyo.

“Wasimamizi wa kanisa hilo wameripoti kuibiwa kwa zana za muziki kama piano, spika na vipaza sauti pamoja na ndarama,” akasema.

Aliongeza kwamba walipokuwa wanaingia kwa Kanisa hilo, waliacha kama wamemshambulia na kumjeruhi bawabu aliyekuwa akililinda na ambaye hatimaye aliaga dunia akitibiwa.

“Maafisa wa uchunguzi wa makosa ya jinai walifika katika kanisa hilo na kutekeleza uchunguzi na ambapo kwa sasa tunasaka washukiwa pamoja na mali iliyoibiwa,” akasema.

Bw James Wairagu ambaye ni jirani wa kanisa hilo aliambia Taifa Leo kwamba alisikia vurugu na kisha mayowe ya bawabu akishambuliwa “lakini sikuthubutu kutoka nje, nilichofanya ni kuandikia afisa wa polisi ninayemjua ujumbe mfupi kwa simu kuhusu uvamizi huo”.

Badala yake, anasema alisongea ukuta na kusikiza yaliyokuwa yakijiri “na niliwasikia wakivuta vitu huku wengine wakisema divai ya Yesu ni tamu na kisha wakatoka wakiwa wanaimba nyimbo za kikiristo…sasa ndio nimejua labda divai ndiyo ilikuwa inawachochea waimbe wakiiba”.

Hasara ambayo Kanisa hilo linakadiriwa ni ya Sh400,000 ambapo Bw Muchiri amesema “tuko na matumaini makuu kwamba tutanasa wavamizi hao na tupate vyombo vya muziki ambavyo waliiba”.

Aliwataka wananchi pamoja na wafanyabiashara wanaouza na kununua vyombo vya aina hiyo wasaidie polisi kuwapata washukiwa ili washtakiwe.

  • Tags

You can share this post!

Seneta Cherargei: Pombe hatari inanonesha watu wembamba

Msanii kutoka Tanzania akana kuzaa Kenya 

T L