• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Murkomen afanya mabadiliko katika usimamizi wa KAA

Murkomen afanya mabadiliko katika usimamizi wa KAA

NA WINNIE ONYANDO

WAZIRI wa Barabara na Uchukuzi, Kipchumba Murkomen amefanya mabadiliko katika usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA).

Akihutubia wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi mnamo Jumamosi, waziri huyo amesema kuwa KAA imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya usimamizi mbaya.

“Mabadiliko hayo yataanza kutumika mara moja. Mabadiliko zaidi yatafuata katika siku zijazo,” akasema Bw Murkomen.

Waziri amesema Bw Alex Gitari, ambaye amekuwa Mkurugenzi Mkuu wa KAA, amekubali kujiondoa na nafasi yake sasa imechukuliwa na Henry Ogoye kama kaimu. Bw Ogoye ndiye afisa wa Uratibu wa Ushirikiano.

Kadhalika, nafasi ya Fred Odawo, ambaye amekuwa Meneja wa Huduma za Miradi na Uhandisi, imechukuliwa na Samuel Mwochache.

Zaidi ya hayo, mabadiliko yafuatayo pia yamefanyika katika usimamizi vya viwanja vya ndege. Abel Gogo, Meneja wa Uwanja wa Ndege wa JKIA atahudumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mombasa. Selina Gor (Kisumu) sasa amepelekwa JKIA, naye Peter Wafula akitolewa Mombasa na kupelekwa Kisumu.

Mabadiliko hayo yanakuja baada ya shughuli kuyumba jana Ijumaa usiku stima zilipopotea na wasafiri uwanjani JKIA, hasa katika Terminal A, ambapo huwa kuna shughuli nyingi, wakajipata gizani.

Waziri Murkomen ameagiza majenereta mawili yaletwe mara moja na yaanze kazi ili hali kama hiyo iliyotokea Ijumaa usiku isitokee tena.

Tayari Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Kawi imeita Waziri wa Kawi Davis Chirchir na Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya Power Joseph Siror, aliye pia Afisa Mkuu Mtendaji, kufika mbele ya wabunge kuelezea kiini cha kupotea kwa stima kote nchini mnamo Ijumaa na Jumamosi.

Waziri Chirchir na Mhandisi Siror wanatarajiwa kufika mbele ya wabunge kuelezea kiini cha kupotea kwa stima kote nchini baada ya Kamati ya Kawi kusema itawahoji wawili hao kuhusu tukio hilo ambalo pia liliathiri Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi ambao ni kitovu wa uchukuzi wa angani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Mwenyekiti ameagiza kwamba tuite Waziri wa Kawi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Power kufika mbele ya wanachama ili wawili hao waelezee kilichosababisha kupotea kwa umeme sehemu nyingi nchini, ikiwemo katika uwanja wa JKIA, na kutatiza wasafiri katika uwanja wenye shughuli nyingi,” ikasema taarifa iliyotolewa na Sekritariati ya Kamati hiyo Jumamosi asubuhi.

Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka almaarufu ‘Kawaya’.

  • Tags

You can share this post!

‘Blackout’ mara mbili kwa wamiliki wa baa...

‘Slay queens’ wadaiwa kuwinda mbegu za...

T L