• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
‘Blackout’ mara mbili kwa wamiliki wa baa wateja wakitokomea gizani bila kulipia bia

‘Blackout’ mara mbili kwa wamiliki wa baa wateja wakitokomea gizani bila kulipia bia

NA RICHARD MAOSI

BAADHI ya wamiliki wa baa na kumbi za burudani kando ya barabara ya Kanu Street viungani mwa jiji la Nakuru wanakadiria hasara tupu baada ya walevi kutimka bila kulipia pombe, vinywaji vingine na minofu Ijumaa usiku.

Hii ni baada ya stima kupotea ghafla mwendo wa saa nne usiku wateja walipokuwa wakiendelea kujiburudisha.

Alice* sio jina halisi, ambaye ni mmoja wa wahudumu katika mojawapo ya kumbi za burudani anasema siku ya Ijumaa kwa kawaida biashara ya pombe eneo la Kanu Street hunoga kutokana na idadi kubwa ya wateja na gharama nafuu ya vyakula.

Anasema stima zilipotea wateja walipokuwa wakitazama mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambapo Chelsea na Luton Town walikabiliana.

Alikuwa akiendelea kuzunguka huku akiwahudumia wateja  pale stima zilipotea.

“Kwa sababu mara nyingi wateja hunywa pombe kabla ya kulipa, baadhi yao walianza kuhepa na hata kuwazidi nguvu mabaunsa waliokuwa wameshika doria. Wateja hao walitoweka kupitia mlango wa nyuma huku wengine wakijificha ndani ya choo wakisubiri mwanya wa kutokea,” akasema.

Amefichulia Taifa Leo kuwa baadhi ya wateja walilazimika kukesha ndani ya baa mpaka asubuhi wakihofia kwamba huenda wangekutana na wahalifu barabarani.

“Eneo la Kanu Street linazungukwa na mitaa ya mabanda ya Bondeni, Kivumbini, Lake View Rhonda na Langa Mwisho na hawakuwa tayari kuporwa,” akasema Alice.

Kulingana naye, hii sio mara ya kwanza jambo kama hili kutokea ndiposa anashauri waliowekeza kwenye biashara ya pombe kusaka njia mbadala ya kawi kama vile jenereta ili kuepuka hasara kama hii.

Mbali na kufurahia muziki, wateja wengi humiminika katika maeneo ya burudani kutazama soka kwenye runinga na kula  nyamachoma.

  • Tags

You can share this post!

Chirchir, Siror waagizwa kufika mbele ya Kamati ya Kawi...

Murkomen afanya mabadiliko katika usimamizi wa KAA

T L