• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Murkomen aondolea Kenya Power lawama za mahangaiko ya JKIA

Murkomen aondolea Kenya Power lawama za mahangaiko ya JKIA

NA WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Uchukuzi, Bw Kipchumba Murkomen, sasa ameiondolea lawama Kampuni ya Kusambaza Nguvu za Umeme Nchini (KP), kutokana na mtindo wa umeme kupotea kila mara katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), jijini Nairobi.

Mnamo Alhamisi, Desemba 14, 2023 Bw Murkomen alitaja tatizo hilo kuchangiwa na miundomsingi duni ya kusambaza umeme katika uwanja huo.

Waziri Murkomen pia alihusisha tatizo hilo na ukosefu wa motisha wa kutosha miongoni mwa wafanyakazi katika uwanja huo na Halmashauri ya Kusimamia Viwanja vya Ndege Kenya (KAA).

“Matatizo ya umeme kupotea kila mara katika uwanja wa JKIA hayahusiani na utendakazi wa KP. Hili ni tatizo lililoanza zamani sana. Limekuwepo hata wakati wa serikali zilizopita,” akasema Bw Murkomen.

Waziri huyo alisema kuwa tiba kuu kwa matatizo hayo ni utengenezaji na ulainishaji wa mitambo ya kusambaza umeme katika uwanja huo, wala si kuielekezea lawama KP kila wakati umeme unapopotea.

“Ingawa kampuni ya Kenya Power ina changamoto zake, tatizo ambalo limekuwa likitokea katika JKIA linahusiana na usimamizi mbaya wa uwanja huo wenyewe wala si la taasisi ya nje,” akasema Bw Murkomen.

Kwa muda mrefu, wasafiri ambao wamekuwa wakijipata gizani katika uwanja huo umeme unapopotea, wamekuwa wakiilaumu kampuni hiyo.

 

  • Tags

You can share this post!

Demu akubali mistari ya jamaa kwa sharti moja: “Utanilipa...

Tanzia mwanamuziki wa Injili akianguka na kufariki...

T L