• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Mwanamume afariki siku moja kabla ya kufunga pingu za maisha

Mwanamume afariki siku moja kabla ya kufunga pingu za maisha

NA MWANGI MUIRURI

POLISI wanachunguza kisa ambapo bwana harusi alipatikana ameaga dunia nyumbani kwake, siku moja kabla ya kufunga pingu za maisha katika Kanisa la Deliverance, Kahawa Sukari, Kaunti ya Kiambu.

Polisi kutoka Kiambu wanashirikiana na wenzao kutoka jijini Nairobi kutegua kitendawili cha Bw Fred Gitau aliyekuwa aamkie ndoa yake na Bi Joyce Waithera mnamo Jumamosi, Agosti 26, 2023 lakini akaaga dunia katika mazingira tata na ambayo yanaashiria aliuawa.

Kamanda wa polisi wa Kiambu Bw Perminus Kioi amesema kwamba uchunguzi kuhusu kisa hicho umeanzishwa kwa ushirikiano na wenzao wa kutoka Kaunti ya Nairobi wanaongozwa na Bw Adams Bungei.

Ripoti ya Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambayo Taifa Leo imeona inaonyesha kwamba marehemu alikuwa ameshinda katika mikutano ya kuimarisha mikakati ya sherehe ya ndoa yake ambayo ilimpeleka maeneo kadha ya Kaunti ya Kiambu na pia Nairobi.

“Mwendazake alikuwa katika mikutano hiyo akiandamana na wandani wake, wakiwemo pia mashahidi wake wakuu wawili katika harusi yake hiyo iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Wawili hao, ripoti yasema, wanadaiwa kuwa ndio walikuwa wa mwisho kuonekana naye na kwamba walimbeba kwa gari lao hadi nyumbani kwake katika mtaa wa Kahawa ulioko Kaunti ya Nairobi.

“Lakini mashahidi wanaeleza kwamba hakuwa na ishara yoyote ya kuwa na afya mbaya na alikuwa mchangamfu huku akitoa ucheshi tele kuhusu siku yake muhimu. Lakini watu wa familia, marafiki na majirani walipigwa na butwaa kupata habari kwamba Bw Gitau alikuwa ameaga dunia kitandani mwake Ijumaa asubuhi,” ripoti hiyo yasema.

Ripoti hiyo inaelezea kwamba mwili wake haukuwa na majeraha ila tu ishara za povu mdomoni.

“Mwili sasa utafanyiwa upasuaji ili ripoti ya kitaalamu iandaliwe na ambayo itatoa mwelekeo kuhusu kiini cha kifo hicho. Kwa sasa uchunguzi unaonyesha aliaga dunia katika hali ya kutatanisha,” ripoti hiyo yaonyesha.

Dokezi kutoka kwa familia ya mwendazake zinadai kwamba Bw Gitau alikuwa akiishi na wasiwasi kwa muda kabla ya mipango ya ndoa yake kuimarika na hata “alikuwa ametoa dokezi kwa dadake kuhusu mshukiwa wa kumtishia maisha.”

Bw Douglas Njiiri ambaye ni mzee wa Kanisa la Deliverance amesema kwamba kwa sasa mambo haya tumeyaachia polisi ili wayachunguze na ni pigo kubwa kwa bibi harusi ambaye tangu habari hizo zitufikie amekuwa akilia kiasi kwamba tumemwasilisha hospitalini ili apate ushauri nasaha na pia matibabu dhidi ya msombo wa kimawazo”.

Alisema kwamba kanisa limetoa ujumbe kwa washirika wake wote washirikiane na maafisa wa polisi katika uchunguzi wa kisa hicho.

“Kila yeyote ambaye ana habari kuhusu kiini cha mauti haya anafaa asaidiane na maafisa wa uchunguzi. Ni suala la huzuni sana,” akasema.

Kasisi Mary Nduta amemtaja mwendazake kama “mwokovu ngangari aliyekuwa na msimamo thabiti kuhusu maisha ya kumtumikia Mungu na hakuwa katika uraibu wa ulevi”.

Amesema kuna baadhi wanaojaribu kupenyeza dhana kwamba Bw Gitau alikuwa ameburudika pombe kabla ya kupelekwa nyumbani kwake.

“Wengine kwa sasa wamezindua misururu ya udaku kuhusu mauti haya. Tunafaa tuwape maafisa wa polisi muda wa kuyachunguza huku nasi tukizidisha maombi kwa Maulana atupe jibu la haki,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

‘Slay queens’ wadaiwa kuwinda mbegu za...

Ababu ataka wabaya wa Azziad wakome kuzua madai ya uongo...

T L