• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Polisi wamzungusha seneta Omtatah akitaka kuandikisha taarifa kwa kuhofia maisha yake

Polisi wamzungusha seneta Omtatah akitaka kuandikisha taarifa kwa kuhofia maisha yake

NA WYCLIFFE NYABERI

SENETA wa Busia Okiya Omtatah amesema anahofia maisha yake kutokana na juhudi zake za kupinga ushuru wa nyumba kupitia utaratibu wa kesi mahakamani.

Seneta huyo mwanaharakati, amedai matamshi aliyoyatoa Rais William Ruto mnamo Desemba 16, 2023, alipohudhuria hafla ya kuchangisha pesa katika Kanisa Katoliki eneo la Mosocho, Kaunti ya Kisii, yalimlenga yeye na Wakenya wengine waliowasilisha mahakamani kesi ya kupinga ushuru huo wa asilimia 1.5 kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi.

Katika makato ya ushuru huo mpya, Wakenya wenye ajira hukatwa asilimia 1.5 ya mshahara wao na waajiri wao pia hukatwa kiasi sawa na hicho.

Wakati wa ziara yake, Rais Ruto alisema: “Si mliona nilipewa upanga wakati nilipoapishwa? Nyinyi mnafikiri ulikuwa wa kukata mboga? Hapana… Ni sime ya kukabiliana na wakora wanaotupeleka kortini kuzuia miradi kama ya nyumba za bei nafuu.”

Ni kauli hiyo ya Rais ambayo Omtatah amesema inamkwaza.

Akihutubia wanahabari mjini Kisii mnamo Jumanne Desemba 19, 2023, seneta huyo pia amesema Rais katika kuongea kwake alitumia maneno ya kuwadunisha watu wanaopinga ushuru huo kama “wakora”.

Bw Omtatah alisimulia jinsi ambavyo juhudi zake za kutaka kuandikisha taarifa kwa polisi kuhusu “kutishiwa maisha kwake” zimekuwa zikisambaratishwa na wakuu wa polisi.

“Mwanzo nilienda katika kituo cha polisi cha Lang’ata kuandikisha taarifa kuhusu hofu ya maisha yangu lakini wakuu wa kituo hicho walinizungusha sana. Lakini alikuja kwangu afisa wa ngazi ya chini na kunieleza kuwa jinsi wenzake walivyokuwa wakiongea, hawangenisaidia kurekodi taarifa. Afisa huyo alinishauri nije Kisii kulikotolewa semi hizo za rais, hata kama zilipeperushwa na vyombo vya habari,” Bw Omtatah akasema.

“Nilijaribu kuagiza usafiri wa ndege kuja Kisii lakini nilielezwa ndege zote zilikuwa zimejaa,” seneta huyo ameongeza.

Alipofika Mosocho vilevile Bw Omtatah alipokezwa makaribisho kama ya Lang’ata, amedai.

Alikwenda hadi kwenye kituo kingine cha polisi cha Nyanchwa lakini hakupata usaidizi wowote.

Anaeleza kuwa alipeleka kesi ya ushuru huo wa nyumba mahakamani hivyo “ninahisi vitisho hivyo vilielekezwa kwangu”.

“Mimi ni mmoja wa wale waliopeleka suala hili mahakamani na ndiyo maana niko hapa kuripoti suala hili kulingana na sheria,” akasema.

Alisema hakuelewa ni kwa nini Kamanda wa Kaunti Ndogo ya Kitutu ya Kati alikataa kurekodi taarifa yake.

“Nilikaribishwa kwa ukarimu na maafisa wa kituo cha polisi cha Mosocho lakini walinituma hapa. Nimesikitishwa kuwa kamanda hawezi kukubali taarifa yangu,” kiongozi huyo akalalamika.

“Lakini mimi ni raia anayetii sheria kuliko hata kiongozi wa nchi,” akasema huku akishikilia kuwa ana kila sababu ya kuamini kwamba maisha yake yako hatarini.
Tayari Chama cha Mawakili Nchini (LSK) kimemsuta Rais Ruto kwa matamshi hayo, kikimwambia akome kutoa vitisho kwa watu wanaopinga sera za serikali.

  • Tags

You can share this post!

Seneta Omtatah ahofia maisha yake

Prof Lonyangapuo: Wanasiasa Pokot Magharibi wameingiwa na...

T L