• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Raila ayakashifu matamshi ya Linturi

Raila ayakashifu matamshi ya Linturi

JUSTUS OCHIENG’ na SIMON CIURI

KINARA wa ODM Raila Odinga jana Jumapili aliwaonya wanasiasa dhidi ya kutoa matamshi ya kichochezi akisema hilo litazua mgawanyiko na uhasama wa kikabila nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Waziri huyo mkuu wa zamani alikashifu matamshi ya uchochezi ya Seneta wa Meru Mithika Linturi wakati wa mkutano wa Naibu Rais Dkt William Ruto mjini Eldoret Jumamosi, akisema si ya heshima na yanaweza kusababisha watu wenye misimamo tofauti kisiasa kuathirika kibaguzi.

Bw Linturi aliwarejelea wanaopinga azma ya Dkt Ruto eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa kama ‘madoadoa’ ila baadaye akakanusha kuwa matamshi yake yalifasiriwa vibaya kwa kuwa alikuwa akiwarejelea wabunge wasioegemea mrengo wa Naibu Rais wala si raia.

Hata hivyo, Bw Odinga ambaye alikuwa akihutubu katika Kanisa la Kianglikana la St John Mwimuto, Kabete Kaunti ya Kiambu, alishikilia kuwa Kenya ni taifa huru na siasa za kuwashurutisha watu wafuate mkondo fulani wa kisiasa zimepitwa na wakati.

“Hatufai kuwarejelea watu kwa kutumia maneno kama kwekwe (magugu) na madoadoa. Hatufai kurejea mahali tulikotokea. Watu wote wanafaa waheshimwe bila kubaguliwa kwa msingi wa dini, kabila, jinsia au umri,” akasema Bw Odinga.

“Hii katiba mpya haikupatikana kwa njia rahisi. Watu walijinyima sana na hatuwezi kuyaruhusu matunda yake yaishe vivi hivi. Lazima tuyakatae matamshi ya chuki na matendo yanayolenga kuwagonganisha raia,” akaongeza.

Kwenye hotuba yake kwa waumini wa kanisa hilo aliwataka Wakenya wajihadhari na wanasiasa ambao sasa wanamakinikia uenezaji wa chuki ili kuwatia hofu ndipo wapigiwe kura.

“Nilisikia mwanasiasa mmoja akizungumzia vibaya watu wenye asili ya kihindi. Waraabu, Wahindi pia ni Wakenya na lazima tuwakubali kama wenzetu. Kila Mkenya anaruhusiwa kuishi mahala popote. Kwa mfano, Mkikuyu anaruhusiwa kuishi Eldoret jinsi tu Mluhya anakubaliwa kuishi Nyeri,” akasema.

Kwa mara nyingine, Bw Odinga aliahidi kuhakikisha kuwa Wakenya wote ambao walipoteza makao yao baada ya ghasia za uchaguzi wa 2007 wanapata makao.

“Kuna watu wengi ambao walipoteza mali na ardhi zao. Hatutaki matukio kama hayo yajirudie. Nitahakikisha kuwa kila Mkenya ambaye alipoteza ardhi yake kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi, anapata makao,” akasema.

You can share this post!

Watano waachiliwa kwa madai ya kubomoa ukuta wa kampuni...

Mudavadi arai maafisa waepuke siasa

T L