• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
George Weah akubali kichapo cha Upinzani   

George Weah akubali kichapo cha Upinzani  

NA WANDERI KAMAU

RAIS George Weah wa Liberia amekubali kushindwa na mwaniaji urais wa Upinzani, Joseph Boakai, kwenye matokeo ya kura yaliyoendelea kutolewa Ijumaa jioni, Novemba 17, 2023 na tume ya uchaguzi nchini humo.

Bw Weah, ambaye alikuwa ameliongoza taifa hilo tangu 2017, alishindwa na Boakai, aliyezoa asilimia 50.9 ya kura huku yeye akipata asilimia 49.1 ya matokeo ya kura yaliyokuwa yametolewa.

Hiyo ilikuwa duru ya pili ya uchaguzi, baada ya mshindi wa moja kwa moja kukosa kupatikana kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 10, 2023.

“Kulingana na matokeo ambayo yametangazwa, ijapokuwa si yote….Yanaonyesha kuwa Boakai anaongoza kwa kiwango ambacho hatuwezi kumfikia,” akasema Bw Weah kwenye hotuba aliyotoa kupitia kituo rasmi cha redio cha serikali.

“Chama cha Congress for Democratic Change (CDC) kimepoteza uchaguzi huo, lakini Liberia imeibuka mshindi. Huu ni wakati wa kuonyesha shukrani hata ikiwa tumeshindwa. Ni wakati wa kuweka mbele maslahi ya kitaifa kuliko ya mtu binafsi,” akasema Rais huyo anayeondoka.

Ushindi wa Bw Boakai unaonekana kuwa kisasi cha kisiasa dhidi ya Weah, kwani alimshinda kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa urais iliyofanyika 2017.

Kulingana na matokeo hayo, Boakai alikuwa akiongoza kwa zaidi ya kura 28, 000.

Amerika ni miongoni mwa mataifa ambayo tayari yametuma ujumbe wa pongezi wa Boakai.

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Barabara yakatika kufuatia mvua na kuacha wanakijiji 3,000...

Mke wa Trossard alia mumewe kuadimika chumbani

T L