• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Barabara yakatika kufuatia mvua na kuacha wanakijiji 3,000 wakikodolea macho njaa

Barabara yakatika kufuatia mvua na kuacha wanakijiji 3,000 wakikodolea macho njaa

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI karibu 3,000 wa vijiji vya Pandanguo na Jima, tarafa ya Witu, Kaunti ya Lamu wanahofia kukumbwa na baa la njaa baada ya barabara yao ya pekee ya Pandanguo-Witu kukatika katika eneo la Ziwa la Kiboko.

Hii ni kufuatia mafuriko yanayochangiwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa eneo hilo kwa karibu juma zima sasa.

Barabara hiyo ya karibu kilomita 21 ni ya changarawe ilhali sehemu zingine zikiwa za mchanga.

Aidha mvua ambayo imekuwa ikinyesha imeacha vidimbwi vya maji chafu vikienea kila mahali, hivyo kuathiri shughuli za uchukuzi.

Ikumbukwe kuwa barabara hiyo ndiyo kiunganishi cha pekee kwa wakazi wa Pandanguo na Jima kufikia maduka na masikonya bidhaa yapatikanayo mji wa Witu kwani vijiji hivyo ni vya mashambani, ikizingatiwa kuwa vimepakana na msitu mkuu wa Boni.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, Mzee wa Nyumba Kumi katika kijiji cha Pandanguo, ambaye pia ni msemaji wa jamii ya walio wachache ya Waboni, Bw Ali Sharuti alisema familia nyingi zimekuwa zikitatizika kupata chakula, ikizingatiwa kuwa eneo la kipekee kujinunulia bidhaa ni mji wa Witu ambao kwa sasa haufikiki kutokana na barabara yao kusombwa na mafuriko.

Bw Sharuti aliiomba serikali kuu kushirikiana na ile ya kitaifa na mashirika, ikiwemo lile la msalaba mwekundu, kuwafikishia misaada ya chakula na vyandarua.

“Tunahofia kuambukizwa maradhi yatokanayo na maji chafu yaliyotapakaa kila mahali kutokana na mvua kubwa inayonyesha. Mbu wako kila mahali. Isitoshe, barabara yetu imekatika kumaanisha hatuwezi kufikia maduka kujinunulia chakula. Twaomba hata kama ni ndege kupitia ufadhili wa kaunti, serikali kuu na mashirika itufikishie vyakula vya msaada, vyandarua na dawa za kutibu maji. Twahofia baa la njaa na mlipuko wa maradhi vijijini mwetu,” akasema Bw Sharuti.

Bi Mariam Musa, mkazi wa Jima alisema baadhi ya familia zimelazimika kugeuka na kuwa ombaomba, wakiishi kupitia usaidizi wa majirani tangu mvua ilipoanza kushuhudiwa.

“Kuna baadhi ya familia zilikuwa zimejiwekea chakula kwenye maghala ilhali nyingine zilipatwa na mafuriko zikiwa bila chochote. Sasa zimekuwa zikiomba msaada kwa majirani wakitarajia kesho itakuwa Sawa. Twaishi kwa nguvu za Mungu hapa. Tunahitaji usaidizi,” akasema Bi Musa.

Wakazi pia wameiomba serikali kuijenga na kuiweka lami barabara yao ya Pandanguo-Witu ili kusitisha mafuriko na mahangaiko ya kila aina kila wakati mvua kubwa inayoshuhudiwa maeneo yao.

Vijiji vya Pandanguo na Jima ni makazi ya jamii ya walio wachache ya Waboni.

  • Tags

You can share this post!

AU yataka vijana watumie teknolojia kutatua shida zao

George Weah akubali kichapo cha Upinzani  

T L