• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Rais Ruto aelekea nchini China kupalilia uhusiano na kuvutia wawekezaji

Rais Ruto aelekea nchini China kupalilia uhusiano na kuvutia wawekezaji

NA LABAAN SHABAAN

RAIS William Ruto amefunga safari ya kuenda nchini China kwa ziara ya siku tatu katika juhudi zake za kuvutia wawekezaji zaidi nchini.

Kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, ziara hii itasisitiza uhusiano dhabiti wa kibiashara kati ya Kenya na China.

Pia itaangazia jinsi nchi imejihusisha na Mpango wa Miundomsingi na Barabara – The Belt and Road Initiative – unaoendeshwa na China almaarufu BRI.

BRI, ni mpango wa kimataifa wa mikakati ya ustawishaji miundombinu ulioanzishwa na serikali ya China 2013.

Taifa hilo la bara Asia lilibuni mfumo huu ili kuwekeza zaidi katika angalau mataifa 150 na mashirika ya kimataifa.

Rais Ruto atahudhuria kongamano la tatu la BRI litakalowaleta pamoja viongozi wa dunia jijini Beijing.

“Mazungumzo yatakayopamba jukwaa hilo ni pamoja na wito wa ushirikiano, zingatio la ustawishaji miundomsingi na kuboresha muunganisho baina ya mabara na watu,” ilisema taarifa ya Bw Hussein.

Kadhalika, msemaji wa ikulu aliweka wazi hotuba ya rais itakayonasa suala la ‘uchumi dijitali kama njia mpya ya ukuaji’.

Hapa, Dkt Ruto anatarajiwa kuangazia hatua ambazo Kenya imepiga katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Uvumbuzi.

Kenya ni moja ya mataifa yaliyonufaika kutoka kwa mpango wa BRI, hasaa kupitia moja ya miradi mikuu ya uchukuzi wa reli ya kisasa maarufu SGR.

Katika ziara hiyo, kiongozi wa taifa atafanya mazungumzo na Rais wa China Xi Jinping na viongozi wengine wa dunia kuhusu masuala ya manufaa kwa mataifa husika.

“Rais vile vile atashiriki mazungumzo ya meza mduara na wawekezaji wa Kenya na China kutilia mkazo nafasi ya Kenya kama kitovu cha uwekezaji kwa kampuni za China, ili kuwezesha ushirikiano wa manufaa kwa mataifa yote mawili na raia wake,” Bw Hussein alisema.

Oktoba 6, 2023, Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema Dkt Ruto angeenda China kuomba mkopo wa Sh150 bilioni kuendeleza miradi ya maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

STAA: MVP Akinyi aliyeshindia Nyamira ubingwa wa hoki

Kwayamasta nusura aharibu ndoa yake ‘mpango’...

T L