• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Ruto afungua jengo la miaka miwili Lamu

Ruto afungua jengo la miaka miwili Lamu

RAIS William Ruto ameongoza hafla ya ufunguzi wa jumba la makao makuu ya Kamishna wa Kaunti ya Lamu, miaka miwili baada ya jengo hilo kuanza kutumiwa.

Jumba hilo la Sh214 milioni tayari lilikuwa likitumika tangu mwaka 2021 baada ya ujenzi wake kukamilika.

Lilijengwa na serikali ya kitaifa kuanzia mwaka wa 2019 hadi 2020 kabla ya kuanza kutumika mapema 2021, hasa baada ya ofisi ya kamishna wa Lamu kuhamishwa kutoka kisiwa cha Lamu hadi Mokowe.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jengo hilo, Dkt Ruto aliwahimiza maafisa wa utawala na idara za serikali kulitumia vyema kwa kuhakikisha wananchi wanapokea huduma za serikali kama ipasavyo.

Idara nyingine za serikali zenye ofisi zake kwenye makao hayo makuu ya kamishna wa kaunti ni zile za usajili wa vitambulisho, kadi za kuzaliwa, kadi za kifo na kadhalika.

“Nafurahia kufungua makao makuu ya kamishna wenu hapa Lamu mjini Mokowe leo. Mbali na kwamba huduma za serikali tunhaziamisha ili kufanywa kidigitali, ni muhimu pia kuwa na afisi za kama hii tuliyofungua leo,” akasema.

Aliongeza: “Lazima maafisa wa utawala watakaohudumu kwenye afisi hii wawajibike kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za serikali bila malalamishi yoyote.”

Wakati wa ziara hiyo, Bw Ruto alikabidhi hundi ya Sh63 milioni kwa jamii ya wavuvi, hatua anayoamini itaboresa na kupanua sekta ya uvuvi eneo kote Lamu.

Pia alisema anafanya mazungumzo kabambe na wawekezaji ili kuona kwamba shughuli za biasara Bandari ya Lamu zinatekelezwa kama ilivyotarajiwa.

Gavana wa Lamu, Bw Issa Timamy, aliahidi kushirikiana na serikali ya kitaifa ili kuhaakikisa maendeleo yanaafikiwa kaunti hiyo na nchini kwa ujumla.

Bw Timamy aliwaponeza wakazi wa Lamu kwa kuepuka kushiriki maandamano ya kupinga gharama ya juu ya maisha.

“Sisi tumekataa kuvaa masufuria kichwani na kuandamana. Hapa Lamu hatujawahi kuwa na maandamano ya upinzani na wala hutaona. Sisi tunashirikiana na serikali kuu ili kuendeleza maendeleo hapa,” akasema Bw Timamy.

Wengine walioandamana na Rais Ruto ni Mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Aisha Jumwa (Utumishi wa Umma, Usawa na Jinsia), Salim Mvurya (Uvuvi na Uchumi wa Baharini), makatibu, wabunge, maseneta na wengineo.

Rais yuko kwa ziara ya siku tano kaunti za Pwani.

Baadaye mchana, alielekea Kaunti ya Tana River ambapo alipokelewa na Gavana Dhadho Godhana, Seneta Danson Mungatana miongoni mwa viongozi wengine.

Alikabidhi Shule ya Msingi ya Marembo Sh1 milioni, akisema ni malipo ya jinsi helikopta yake ilitua katika uwanja wa shule hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Mawaziri waimiminia Lamu sifa kwa kukataa maandamano

Wapwani wamtunuka sifa Rais Ruto

T L