• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Wapwani wamtunuka sifa Rais Ruto

Wapwani wamtunuka sifa Rais Ruto

NA KALUME KAZUNGU

AHADI nono za Rais William Ruto kwa Kaunti za Pwani zinazidi kufufua matumaini miongoni mwa wananchi wanaodai kuwa endapo zitatimizwa, basi Ukanda wa Pwani utakuwa eneo bora la kuishi.

Katika ziara yake Lamu Alhamisi, Rais Ruto alifichua kuwa serikali yake tayari inafanya juu chini kuboresha sekta kadhaa ambazo ni uti wa mgongo kwa uchumi wa kaunti za Pwani, hasa uvuvi.

Kwa mujibu wa Rais Ruto, takriban Sh550 milioni zitakabidhiwa sekta ya uvuvi kwa kaunti za Pwani kwenye ziara yake ya siku tano eneo hilo kwa minajili ya kupanua sekta hiyo muhimu ambayo imeajiri wakazi wengi.

Bw Ruto alisema baadhi ya fedha hizo zitaendea makundi ya wavuvi, hasa kwenye kaunti za Lamu, Tana River, Kilifi, Mombasa na Kwale, ambapo makundi ya kijamii ya wavuvi Lamu tayari yalishakabidhiwa Sh63 milioni kuboresha shughuli zao.

Alisema serikali kwa ushirikiano na kaunti ya Lamu itatekeleza ujenzi wa eneo la maegesho ya wavuvi la Mokowe kwa kima cha Sh100 milioni, ambapo Rais Ruto alimtaka gavana, Issa Timamy kushughulikia utatuzi wa utata uliopo wa ardhi ili mradi uliopangwa utekelezwe mara moja.

“Twataka fedha za uvuvi na uchumi wa baharini ambazo ni karibu Sh550 milioni zitumike kununua vifaa vya kisasa vya uvuvi, majokofu ya kuhifadhia samaki, kuboresha viwanda vya samaki na masuala mengine hapa Lamu na kaunti zingine za Pwani ya Kenya. Azma yangu ni kuipanua hii sekta ya uvuvi miaka ijayo, ambapo badala ya kuleta Sh20 bilioni za pato la samaki, nataka iwe sekta itakayoletea Kenya Sh120 bilioni kutokana na uuzaji wa pato la samaki kila mwaka,” akasema Dkt Ruto.

Alisema serikali kuu ni kuboresha miundomsingi inayoambatana na uvuvi, akitaja kuwa Sh300 milioni tayari zitatolewa mwezi huu kushughulikia ukarabati na uendelezaji wa ujenzi wa maegesho makuu ya samaki ya Liwatoni, kaunti ya Mombasa.

Aliwasisitizia wavuvi na watumiaji wa bahari Pwani na Kenya kwa ujumla kuwajibika katika kuona kwamba uvuvi unapanuliwa vilivyo.

Alhamisi, Rais Ruto aliwapokeza mabaharia wa Lamu (manahodha) 300 leseni za kutekelezea shughuli zao baharini na kujipatia pato bila kusumbuliwa.

Alisema mpango huo utaendelezwa kwa kaunti nyingine hadi pale mabaharia wote zaidi ya 2,000 kwenye maji ya Kenya watakapopokea vyeti hivyo vya idhini ya utendakazi wao.

“Tunatoa leseni hizi baada ya mabaharia kupitia mafunzo muhimu yaliyodhaminiwa na serikali. Leo tunapeana leseni kwa mabaharia 300 hapa Lamu. Tutaendeleza mpango huo wa mafunzo na utioaji leseni kwa mabaharia wote zaidi ya 2,000 Kenya,” akasema Bw Ruto.

Akigusia suala la nyumba za bei nafuu, Rais Ruto alisema yuko imara kushirikiana na kaunti mbalimbali nchini, zikiwemo za Pwani ili kuhakikisha mpango huo unafaulishwa.

Alisema kufikia Desemba, yeye atarudi Lamu kuzindua mpango wa nyumba za bei nafuu, akitaja kuwa tayari ardhi ya kutekelezea mradi huo imepatikana.

“Mpango wa Nyumba za bei nafuu utaleta ajira tele kwa vijana hapa Lamu. Isitoshe, nitashirikiana na magavana, ikiwemo Issa Timamy wa Lamu ili kuendeleza mpango wa kujenga miji ya kisasa ya kiviwanda katika kila kaunti. Gavana wa Lamu tayari ametenga Sh100 milioni kufanikisha mpango huo. Mimi pia kama serikali kuu nitatoa Sh250 milioni kupiga jeki kufaulu kwa mpango huo,” akasema Rais Ruto.

Akigusia suala la Bandari ya Lamu, Rais Ruto alisema serikali kuu kufikia wiki ijayo itatangaza tenda ya kimataifa ili kuwezesha bandari ya Lamu kutekeleza biashara ipasavyo, sawasawa na hadhi yake ya kuwa bandari ya pili kubwa nchini.

Alisema mipango pia ipo ya kuweka lami barabara kuu ya Lamu-Garisa-Isiolo ili kufanikisha shughuli za uchukuzi kutoka bandari ya Lamu hadi nchi za nje.

Viongozi wa Pwani walionyesha matumaini yao kwa juhudi za serikali kuu katika kuboresha hali ya uchumi wa Baharini Pwani.

Gavana wa Lamu, Issa Timamy aliahidi ushirikiano wake na serikali kuu ili maendeleo yaafikiwe Lamu, Pwani na Kenya kwa ujumla.

“Mimi nikiwa mwenyekiti wa Uchumi wa Baharini kwenye baraza la magavana (CoG), ninaunga mkono mipango iliyopo, hasa kwa sekta ya uvuvi Pwani. Ninaamini tukishirikiana vilivyo na Rais wetu, magtunda haya kamwe hayatatupita,” akasema Bw Timamy.

Waziri wa Uvuvi na Uchumi wa Bahari, ambaye zamani alikuwa gavana wa Kwale, Salim Mvurya, alisema yuko na imani na uongozi wa Rais Ruto kwamba maendeleo yote yanayopangwa Pwani na Kenya yataafikiwa.

“Rais Ruto ni mchapakazi si haba. Niko na imani kubwa kwamba ahadi zote anazotoa kwa Ukanda wa Pwani na nchini zitatekelezwa. Tayari tumeona matunda ya uongozi wa Rais Ruto,” akasema Bw Mvurya.

Waziri wa Masuala ya Umma, Usawa na Jinsia, Aisha Jumwa, alimtaja Rais Ruto kuwa kiongozi na wala si mwanasiasa kama wengine nchini.

Aliwasihi Wapwani kuunga mkono serikali ya Rais Ruto, akisema tawala nyingine zilizopita nchini zilikuwa zikibagua Pwani.

“Ruto amedhihirisha upendo wake kwetu sisi Wapwani. Yeye huzuru kila kaunti Pwani kila wakati kinyume na tawala zile zingine zilizopita ambazo zilitubagua,” akasema Bi Jumwa.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na Taifa Leo pia hawakuficha furaha yao kufuatia upendo anaodhihirisha Rais Ruto kwa Wapwani.

“Sisi tuko imara na Rais Ruto. Ndiye Rais ambaye amekuwa karibu sana na sisi wakazi wa Pwani. Tunaamini ahadi zote alizotoa endapo zitatimizwa basi umaskini na mahangaiko tuliyo nayo vitakuwa ni ndoto,” akasema Mzee Kibwana Shali, ambaye ni mvuvi.

  • Tags

You can share this post!

Ruto afungua jengo la miaka miwili Lamu

Wajumbe 3 wa mapatano

T L