• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Ruto aondoa hitaji la visa kwa raia wa Angola

Ruto aondoa hitaji la visa kwa raia wa Angola

NA CECIL ODONGO

RAIS William Ruto ameonekana kuimarisha uhusiano wa Kenya na Angola baada ya kuondoa hitaji la kupata visa kwa raia wa taifa hilo wanaofika nchini.

Kenya na Angola pia zitaimarisha uhusiano wao kwenye Kilimo pamoja na sekta nyingine ya uchumi kwa mujibu wa kiongozi wa nchi.

Rais alikuwa akizungumza Jumamosi katika Ikulu ya Nairobi wakati wa ziara ya Rais wa Angola Joao Lourenco.

Rais huyo wa Angola alistahili kuwa mgeni wa heshima kwenye sherehe za Mashujaa mnamo Ijumaa lakini akawakilishwa na Waziri wa Masuala ya Kigeni Antonio Tete na sababu hasa ya kukosa kwake bado ni kitendawili.

“Rais Lourenco na mimi tunakubaliana kuwa tunastahili kuhakikisha watu wetu wanatangamana na pia kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya Angola na Kenya. Kenya imeondoa hitaji la visa kwa raia wote wa Angola mara moja,” akasema Rais Ruto.

Hata hivyo, serikali ya Angola haikusema iwapo imechukua hatua hiyo kwa raia wa Kenya wanaosafiri Angola. Rais Ruto alifichua kuwa kwenye majadiliano yao, Rais Lourenco alimhakikishia kuwa watazungumzia suala hilo kwao kabla ya kufichua msimamo wao.

Viongozi hao pia walishuhudia kutiwa saini kwa mikataba 11 ya maelewano ambayo itahakikisha kuwa Kenya na Angola zina uhusiano wa kuridhisha. Kwenye sekta ya Kilimo, wakulima nchini watashirikiana na wenzao kuendeleza kilimo ili wapate chakula kwa mataifa ya nchi hizo mbili.

“Hapa Kenya hatuna ardhi yenye rutuba kama Angola. Kuna pendekezo kuwa wakulima kutoka Kenya washirikiane na wenzao kutoka Angola ili kukuza chakula kwa raia wa nchi hizo mbili. Kuna nafasi kubwa ya ushirikiano,” akaongeza Rais.

Baada ya ziara hiyo ya ikulu, kiongozi huyo wa Angola alitembelea kaburi la Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta katika majengo ya bunge na kuweka shada la maua. Kenya ambayo ilipata uhuru wake mnamo 1963, ilichangia sana Angola kupata uhuru wake mnamo 1975 kutoka Ureno.

Pia Kenya na Angola zitashirikiana kutatua mgogoro kule Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Sudan.

Waliomba mirengo inayozozana kwenye mataifa hayo kukubali kuridhiana na kupata muafaka.

  • Tags

You can share this post!

Pasta aweka Biblia kando na kumlima polo aliyemtorosha mkewe

KCB RFC wapiga Oilers kujikatia tiketi ya fainali ya Impala...

T L