• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Ruto: Kenyatta aliacha ghala tupu hata panya walilitoroka

Ruto: Kenyatta aliacha ghala tupu hata panya walilitoroka

NA BARNABAS BII

RAIS William Ruto Ijumaa, Desemba 22, 2023 alisema nafasi aliyopata ya kuliongoza taifa hili ni sehemu ya utabiri wa wazee wa jamii ya Wakalenjin kuhusu ufanisi wa kundi la rika lake la Kaplelach, “atakapotwaa uongozi wa taifa hili”.

Akiongea nyumbani kwaka katika eneo la Sugoi, Turbo, Kaunti ya Uasin Gishu, Dkt Ruto alieleza kuwa sasa ni wajibu wake kuiwezesha nchi hii kupata ufanisi au iangamie.

“Mimi ni mmoja wa wanachama wa rika la Kaplelach na ni fahari yangu kujitambulisha nao na kuchangia kutimia kwa utabiri wa wazee kwamba mmoja wetu ama atastawisha Kenya au ataiporomosha,” Dkt Ruto akaambia umati mkubwa wa watu waliokongamana nyumbani kwake eneobunge la Turbo.

Alisema hayo jana, Ijumaa alipoandaa dhifa ya Krismasi kwa wakazi wa Uasin Gishu nyumbani kwake Sugoi.

Dkt Ruto alitumia fursa hiyo kumshambulia mtangulizi wake Uhuru Kenyatta akisema rais huyo mstaafu alimrithisha hazina ya serikali isiyo na pesa zozote, akiilinganisha na ghala ambalo limetorokwa hata na panya.

Alisema kwa muda wa miezi 15 ambayo ameshikilia wadhifa huo, amefaulu kurejesha imani ya wawekezaji, hali ambayo imefufua uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

“Mnajua yale ambayo reggae na watu wa BBI walifanya kwa uchumi wetu. Nilipoingia afisini hakukuwa na chochote kwenye ghala, hata panya walikuwa wamelitoroka.

“Tangu wakati huo nimefaulu kushawishi washirika wetu wa kimaendeleo na tumefufua uchumi licha ya kukosolewa na wapinzani wetu,” akasema Dkt Ruto.

Mpango wa mageuzi ya katiba kupitia mchakato wa maridhiano (BBI) uliungwa mkono na Bw Kenyatta na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga.

Mahakama, hata hivyo, iliupiga breki.

Hatua hiyo ilimfaidi pakubwa Dkt Ruto aliyetumia uamuzi huo kujipigia kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais Ruto aliambia wakazi wa Uasin Gishu kuwa yu katika tapo la viongozi ambao nia yao kuu ni kustawisha taifa hili.

Rais ambaye alikuwa ameandamana na Mkewe Rachel Ruto, alisambaza zawadi mbalimbali kwa wakazi hao. Miongoni mwa zawadi hizo ilikuwa; unga wa mahindi, unga wa ngano, mchele, sukari, mafuta ya kupikia miongoni mwa bidha nyinginezo.

Bidhaa hizo zilikuwa ni zawadi ya Krismasi kwa wakazi hao.

Dkt Ruto aidha, alitumia nafasi hiyo kukariri kujitolea kwa serikali yake kupunguza gharama ya matibabu kupitia Sheria za kufanikisha Mpango wa Afya kwa Wote (UHC).

“Chini ya sheria hii wale raia wasio na ajira ambao wamekuwa wakilipa ada ya Sh500 kwa mwezi kama mchango wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) sasa watalipa Sh300 pekee na kutibiwa maradhi yote yakiwemo Kansa,” Rais akaahidi.

Dkt Ruto alisema ni makosa kwa watu fulani kuwenda kortini kusitisha miradi inayolenga kuimarisha maisha ya Wakenya kama vile mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

“Chini ya mpango wa ujenzi wa nyumba, nyumba 200,000 zitajengwa kila mwaka. Kufikia sasa zaidi ya watu 12,000 wameajiriwa katika maeneo 31 kunakojengwa nyumba hizo,” akasema Rais Ruto.

 

  • Tags

You can share this post!

Kanisa lasisitiza umuhimu wa elimu ya ngumbaru kuzima...

Nitainua nchi au tuzame, Ruto asema

T L