• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Sabina Chege atakiwa kurejesha pesa alizolipwa bungeni

Sabina Chege atakiwa kurejesha pesa alizolipwa bungeni

NA SAM KIPLAGAT

MUUNGANO wa Azimio La Umoja One Kenya unamtaka Sabina Chege kulazimishwa kurejesha pesa alizolipwa akishikilia wadhifa wa Naibu Kiranja wa Wachache.

Kando na hayo, muungano huo unaitaka Mahakama ya Juu kuufutilia mbali wadhifa huo.

Katika uamuzi wake, Spika wa Bunge la Kitaifa Bw Moses Wetang’ula alitambua Jubilee kama chama kinachojisimamia bungeni na hata kumteua Bi Chege kuwa Naibu Kiranja wa Wachache.

Hata hivyo, muungano wa Azimio unadai kuwa hatua ya kumpa Bi Chege wadhifa huo wakati akiwa mwanachama wa muungano huo ni utumizi mbaya wa fedha za umma na kwa hivyo, ni kinyume cha Katiba.

“Mlalamishi anadai kwamba hatua ya mlalamikiwa kutambua Jubilee kama chama kinachojisimamia Bungeni inadhihirisha kuondolewa kwa chama hicho kutoka kwa muungano wa waliowasilisha maombi bila kufuata utaratibu uliowekwa,” Bw Wycliffe Oparanya, mwenyekiti wa baraza kuu la muungano wa kitaifa wa Azimio alisema.

Azimio inadai kuwa utambuzi huo sio wa haki kiutaratibu, na kwamba unazuia upatikanaji wa haki na ni kinyume cha Katiba.

Chama cha upinzani pia kinasema kuwa kutambuliwa kwa Jubilee kama chama kinachojisimamia bungeni na kutelekeza vyama vingine ni ubaguzi na kinyume cha Katiba.

Aprili 13 2023, Azimio ilimwandikia Bw Wetang’ula kuwasilisha azimio lake kumwondoa Bi Chege kama Naibu Kinara wa Wachache.

Bw Wetang’ula wakati uo huo alidokeza kuwa amepokea ombi kutoka kwa mrengo huo wa upinzani kutaka chama cha Jubilee kitambuliwe kama chama kinachojisimamia bungeni.

Bw Oparanya alidokeza kuwa mizozo ndani ya chama cha Jubilee kuhusu mirengo tofauti inaweza tu kusuluhishwa na Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa chama hicho na kwa ufahamu wake, hakujakuwa na mkutano au kongamano kama hilo.

“Kwa sababu hiyo, chama cha Jubilee hakijawahi kujiondoa kuwa mwanachama wa Muungano wa Azimio la Umoja,” akasema.

Alisema katika hali hiyo, Chama cha Jubilee hakiwezi kutambuliwa kama chama kinachojisimamia bungeni kwani hiyo itakuwa sawa na kuhujumu makubaliano ya muungano kati ya vyama.

 

  • Tags

You can share this post!

Man United ni ‘Mungu Saidia’ ikialika...

Viongozi Mombasa wasusia sherehe ya Jamhuri Dei

T L