• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
Serikali yajipata katika njia panda, ikiwarai Wakenya kutafuta ajira ng’ambo

Serikali yajipata katika njia panda, ikiwarai Wakenya kutafuta ajira ng’ambo

NA WANDERI KAMAU

MTINDO mpya wa serikali ya Kenya Kwanza kutangaza uwepo wa maelfu ya nafasi za kazi katika mataifa ya nje, umeibua maswali kuhusu lengo lake kwa Wakenya.

Tangu Januari 2023, serikali imetangaza kutia saini mkataba na karibu nchi tatu kuwawezesha Wakenya kusafiri katika mataifa hayo kutafuta ajira. Nchi hizo ni Canada, Ujerumani na Amerika.

Mnamo Mei 2, 2023, Rais William Ruto alisema kuwa Kenya na Canada zinabuni mkakati utakaowawezesha wataalamu wa afya kutoka nchini kuenda Canada kwa nafasi za kazi na kuongeza ujuzi wao wa matibabu.

“Wafanyakazi kutoka Kenya huwa na mchango mkubwa kwa ustawi wa nchi. Wana bidii na ujuzi wa kiwango cha juu. Hata tunapowekeza kwenye sekta zitakazobuni ajira, nafasi zilizopo katika mataifa ya nje ni njia nyingine ya kuwainua vijana,” akasema Dkt Ruto.

Alisema hayo alipokutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Canada, Melanie Joly.

Baadaye, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Dkt Alfred Mutua alitangaza kuhusu uwepo wa maelfu ya nafasi za kazi nchini Canada, akiwarai Wakenya kutuma maombi yao.

Hata hivyo, Kenya na Canada zilitoa onyo kwa Wakenya kutahadhari kulaghaiwa na mawakala tapeli kuhusu ajira hizo.

Mnamo Mei 5, Rais Ruto alitangaza tena uwepo wa zaidi ya nafasi 250,000 za ajira kwa Wakenya nchini Ujerumani.

Dkt Ruto alitoa kauli hiyo baada ya kukutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliyekuwa katika ziara nchini.

Rais Ruto alitangaza hayo kwenye kikao cha pamoja na wanahabari katika Ikulu ya Nairobi.

Mnamo Jumapili, Oktoba 1, 2023, Rais Ruto alitangaza kwamba kampuni kubwa za kiteknolojia duniani kama Google, Intel na Apple zinataka kuwaajiri Wakenya.

Rais alisema kuwa tangazo la kampuni hizo linalingana na manifesto ya serikali ya Kenya Kwanza ya kupanua mpenyo wa kiteknolojia nchini.

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wa masuala ya kiuchumi wanasema huenda hatua ya serikali inatokana na kuongezeka kwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, mwanauchumi Tony Watima anasema ni kinaya serikali kuwaeleza raia wake kuhusu nafasi za kazi zilizo katika mataifa ya nje, ilhali inafaa kubuni mikakati ya kubuni ajira katika nchi yake.

“Kilicho wazi ni kuwa Rais Ruto amejipata kwenye njia panda kuhusu jinsi atakavyotatua tatizo la kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini, hasa miongoni mwa vijana. Hilo ndilo linamfanya kubuni mikataba na baadhi ya nchi zenye chumi thabiti kama njia ya kuwasaidia Wakenya kupata ajira ng’ambo,” akaeleza mwanauchumi huyo.

Anasema kuwa hilo ndilo linaonekana kuwa moja ya lengo kuu la ziara nyingi za nje anazofanya Rais Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Ifahamu ngoma maalumu ya kujivunia ubikira wa wanawake wa...

Hisia mseto makundi ya WhatsApp yakijadili suala la maeneo...

T L