• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Ifahamu ngoma maalumu ya kujivunia ubikira wa wanawake wa Uswahilini

Ifahamu ngoma maalumu ya kujivunia ubikira wa wanawake wa Uswahilini

NA KALUME KAZUNGU

KWA miaka mingi ngoma imesalia kuwa njia mwafaka ya waja kuhifadhi utamaduni.

Ni kupitia ngoma ambapo jamii nyingi zimefaulu pakubwa kupitisha mila, tamaduni na desturi kutoka kizazi hadi kizazi.

Katika Kaunti ya Lamu na Pwani kwa ujumla, ngoma, hasa ile ya Vugo, imekuwa changizo kubwa katika kutumbuiza na pia kuhifadhi mila na tamaduni za jamii ya Waswahili wa asili ya Kibajuni.

Ngoma hiyo ya jadi chimbuko lake ni kisiwa cha Faza, Lamu Mashariki.

Ni ngoma ambayo ni maarufu si haba Uswahilini.

Kila inapochezwa, ngoma hiyo hushirikisha wanawake pekee.

Ngoma hiyo huchezwa sana katika sherehe mbalimbali za jamii ya Waswahili Wabajuni, zikiwemo harusi, siku za kuzaliwa, tohara na hata wakati wa kutoa posa.

Vugo pia hutumiwa wakati bwana harusi hufika kuwasilisha zawadi ambapo shukrani na sifa kwa wakwe huwafikia kwa njia spesheli. Hii ina maana kuwa ngoma hiyo kwa sherehe hiyo huwa ni ya kusifu akina mama na shangazi kwa kutunza vizuri mrembo wake, baada ya mume huyo kung’amua kuwa msichana aliyeoa alimpata akiwa ni bikira.

Wengi huishabihia ngoma ya Vugo na ile ya sitara ambayo mara nyingi hutumika kuwasifu wanawali au mabikira.

Ujumbe unaotumwa kwa wakwe kuwasilisha sifa hizo hucheza vugo usiku kucha kwa boma alilozaliwa bibi harusi.

Pia hutumiwa kuwakaribisha wageni wa heshima, hasa wafalme.

Nyakati za sasa, ngoma ya vugo pia imekuwa ikitumiwa kuburudisha wakati wa hafla za kitamaduni, kidini na kitaifa.

Bi Halima Abdallah, mkazi wa kisiwa cha Faza na mchezaji maarufu wa ngoma ya vugo, alieleza kuwa zamani hakukuwa na maeneo mengine yaliyotambuliwa kwa uchezaji wa vugo isipokuwa kisiwa cha Faza.

“Nakumbuka enzi au zama hizo, Vugo ilikuwa ikichukuliwa kama klabu au chama. Utapata wanachama wa vugo kutoka hapa Faza walikuwa wakialikwa kutumbuiza wakati wa hafla za kitamaduni kama harusi zilizokuwa zikifanyika visiwa vya mbali, ikiwemo Kizingitini, Siyu, Pate, Ndau nakadhalika. Ni kutokana na hilo ambapo jamii ilianza kuiga, hivyo kuiwezesha ngoma ya vugo kusambaa kote. Mbali na Lamu, utaipata ngoma hii ikichezwa hata Mombasa na miji mingine ya mwambao wa Pwani,” akasema Bi Abdallah.

Miongoni mwa ala za muziki zinazotumiwa katika densi ya Vugo ni pembe, kijiti, ngoma, twari (thwari), na sinia.

Katibu wa Wizara ya Uchumi wa Baharini, Bi Betsy Muthoni, wakati akitumbuizwa na hata kushiriki ngoma ya Vugo katika sherehe iliyoandaliwa kisiwani Lamu akiandamana na wanawake Waswahili wa asili ya Wabajuni. Ngoma ya Vugo ni maarufu Uswahilini, ikishirikisha wanawake. PICHA | KALUME KAZUNGU

Fatma Alwy anasema wanaocheza ngoma ya Vugo mara nyingi huzingatia heshima katika kunengua au kuimba nyimbo husika.

Bi Alwy anasema kukamilika kwa Vugo au pale Vugo inapoonekana kukolea ni wakati kunapokuwa na mwimbaji mkuu (ngoi), muitikiaji wa nyimbo, mpiga ngoma hodari, wapiga pembe na vijiti na pia wale wanaopiga twari kwa uhodari na kufanya vifaa hivyo vyote vya muziki kuingiliana vyema.

“Vugo ni ngoma tamu inayoburudisha nafsi na kusahaulisha waja presha za ulimwengu. Furaha ya ngoma hiyo ni ni jinsi washirika wanavyoitikia nyimbo wakati ngoi anapowaongoza. Kila ngoi anapomba, waandamizi wanastahili wawe wenye kuitikia ipasavyo ilhali ngoma, pembe na twari zikipigwa ziwe zinaingiliana vyema. Pia kuwe na wanaoshangilia. Hilo likitendeka basi utajipata hata kama huifahamu hii ngoma unasimama mwenyewe kama mwanamke na kucheza bila kujali,” akasema Bi Alwy.

Mbali nyimbo, mashairi sufufu pia hushirikishwa wakati ngoma ya Vugo inapochezwa.

Mbali na wanawake walioolewa ambao mara nyingi huwasilisha ngoma ya Vugo, wasichana wadogo pia hukubalika kushiriki ngoma hiyo ya vugo katika harakati za kuhakikisha Sanaa hiyo inapitishwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine ili isiangamie.

“Utapata wahusika wakiimba au kughani mashairi yenye mahaba wakati wa kuwasilisha ngoma ya vugo. Ngoma hii huwa ni yenye heshima kwani mbali na wanawake walioolewa, wasichana wadogo pia mara nhyingine husirikishwa,” akasema Bw Muhashiam Famau, mzee wa Lamu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mohamed Mbwana Shee alieleza wasiwasi wake kwamba huenda uasilia wa ngoma ya vugo ukaangamia miaka ijayo.

Bw Mbwana anasema miaka ya hivi punde kumeshuhudiwa kila mtu akijihusisha kwenye ngoma ya vugo, ikiwemo wanaume, hali ambayo inaondoa ladha ya burudani hilo.

Wosia wake kwa jamii ya Waswahili Wabajuni ni kwamba kuteuliwa wasichana maalum ambao watapitia mafunzi ya ngoma ya vugo ili kusaidia kuwafunza wenzao na kuirithisha ngoma hiyo kwa vizazi vijavyo ili isiangamie.

“Watu wamekuwa hawafuati sheria tena wanapowasilisha vugo. Utapata wanawake wakicheza vugo ilhali wanaume wakipiga ngoma au twari. Hii ni ngoma ya wanawake na kujumuisha wanaume ni hatua inayokinzana na uasilia wa densi hiyo ya vugo,” akasema Bw Mbwana.

  • Tags

You can share this post!

Weledi wa demu wangu chumbani umenitia wasiwasi

Serikali yajipata katika njia panda, ikiwarai Wakenya...

T L