• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Miguna Miguna adai serikali imemzuia kurejea nchini

Miguna Miguna adai serikali imemzuia kurejea nchini

Na CHARLES WASONGA

WAKILI Miguna Miguna sasa anadai kuwa serikali imemzuia kurejea nchini kwa kuagiza mashirika ya ndege ya kigeni kutomsafirisha.

Kwenye taarifa aliyotuma kupitia ukurasa wa mtandao wake wa Facebook, Miguna alidai kuwa ndege ya shirika la ndege la Air France la Ufaransa – AF 836 – ilikataa kumsafirisha kutoka Ujerumani hadi Nairobi.

“Niko katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Brandenburg. Nimezuiwa kuabiri ndege ya shirika la ndege la Air France kutokana na marufuku kutoka Ikulu ya Rais Uhuru Kenyatta leo (Jumatatu) asubuhi. Wananiogopa kwa sababu umaarufu wao umedorora. Nitaendelea kuwapasha,” Bw Miguna akaandika.

Aliendelea kuonyesha barua ambayo alipewa na shirika hilo la ndege iliyoonyesha kuwa amezuiwa kuiabiri kutokana na marufuku hayo maarufu kama “red alert”.

“Wamesema kuwa wananihurumia lakini hawajui vile watakavyonisaidia. Mawakili wangu waanze kazi. Asanteni kwa kuniunga mkono. Aluta continua,” Miguna akaongeza.

Wakili huyo ambaye amekuwa akiishi uhamishoni nchini Canada alikuwa ametangaza kuwasili nchini Jumanne Novemba 16 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi.

Mwezi jana, Jaji Mkuu Mstaafu Willy Mutunga na Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Nelson Havi walikuwa wameahidi kusafiri hadi Canada kuandamana na Bw Miguna katika safari yake ya kurejea Kenya.

“Uamuzi wangu niliufikia baada ya kutafakari kwa kina. Vile vile, nilifikia uamuzi huo baada ya kufanya mashauriano ya kina na mawakili, watetezi wa haki za kibinadamu, wanasiasa wenye maono endelevu na Miguna mwenyewe,” akasema Bw Mutunga.

Hata hivyo, Jaji huyo Mkuu wa zamani hakusafiri hadi Canada alivyoahidi kwani hakuonekana pamoja na Miguna katika picha ambazo wakili huyo alisambaza mitandaoni tangu alipotoka Canada na kuwasili Ujerumani.

Naye wakili Havi alikuwa jijini Nairobi Jumatatu siku ambayo Bw Miguna alitangaza kuzuiwa kuabiri ndege ya kutoka Ujerumani kupitia Ufaransa kisha Nairobi.

Bw Havi alikuwa miongoni mwa mawakili kadhaa waliofika katika Mahakama Kuu eneo la Milimani, kumwakilisha aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa aliyeshtakiwa kwa ufisadi.

Hili ni jaribio la tatu la Miguna kurejea Kenya kutibuka kutokana na marufuku yaliyowekwa na serikali.

You can share this post!

Samaki azua hofu, akikuuma huonani na mke miezi 6

Dereva chipukizi Yuvraj alenga changamoto mpya kwenye...

T L