• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Serikali yazindua awamu ya pili ya usajili kwa mpango wa ‘Inua Jamii’

Serikali yazindua awamu ya pili ya usajili kwa mpango wa ‘Inua Jamii’

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI inalenga kusajili watu 5,000 kwa mpango wa kuwasaidia wanyonge katika jamii maarufu kama ‘Inua Jamii’.

Miongoni mwa makundi lengwa ni wakongwe, mayatima na watu wanaoishi na aina mbalimbali za ulemavu.

Kwenye taarifa aliyoitoa Jumamosi, Septemba 2, 2023, Katibu katika Wizara ya Leba na Masilahi ya Kijamii Joseph Motari, alisema shughuli hiyo inalandana na lengo la wizara hiyo la kupunguza umaskini na kuimarisha maisha ya wahusika kulingana na sera ya serikali ya Kenya Kwanza ya kufanikisha maendeleo kuanzia ngazi za mashinani (BETA).

Wazee watakaosajiliwa katika awamu hii ya pili ya usajili ni wale wenye umri wa miaka 70 kwenda juu na wanaozongwa na umaskini.

Aidha, mayatima na walemavu watakaosajiliwa ni wale watakaithibitishwa kuwa na uhitaji wa msaada.

“Usajili huo utaendelea kwa siku 20 kote nchini. Watakaosajiliwa watajumuishwa kwenye orodha ya zamani na watakuwa wakipokea Sh2,000 kila mwezi kama marupurupu ya kuwafaa,” Bw Motari akasema.

Katibu huyo wa wizara alisema kuwa usajili huo utafanyika katika afisi za maafisa wa maendeleo ya kijamii katika ngazi za kaunti ndogo.

Wale wanaohitimu kwa usajili katika mpango huo wa Inua Jamii wametakiwa kuwasilisha vitambulisho vya kitaifa na nakala za stakabadhi zitakazohitajika.

“Tunatoa wito kwa wakongwe ambao hawajajisajili kwa mpango huu na walezi wa mayatima na walemavu kutumia nafasi hii kujitokezwa kwa usajili katika afisi husika za serikali,” Bw Motari akashauri.

Katibu huyo alisema serikali imejitolea kuhakikisha kuwa malipo ya wanaofaidi chini ya mpango huo wanalipwa kila mwezi bila kuchelewa, kulingana na agizo la Rais William Ruto.

Malipo ya mwezi Agosti tayari yametolewa kwa wahusika.

Usajili huu wa awamu ya pili ya mpango wa Inua Jamii inajiri kufuatia hatua ya Baraza la Mawaziri kuidhinisha usajili wa watu 500,000 kwa mpango huo katika mwaka wa kifedha wa 2023/2023.

Kufikia Julai 2023, jumla ya watu 1,042,864 walikuwa wakifaidi kwa mpango huo kati ya idadi lengwa ya watu 1,233,129.

Akiongea wakati wa Kongamano la Masilahi ya Kijamii lililofanyika mnamo Aprili 2023, Rais Ruto alielezea kujitolea kwa serikali kuongeza idadi ya watakaofaidi kutokana na mpango wa Inua Jamii hadi kufikia watu 2.5 milioni baada ya miaka mitatu ijayo.

  • Tags

You can share this post!

Bei za bidhaa zingali juu licha ya mvua, takwimu rasmi za...

Karen Nyamu: Ninaomba Mungu abadili ajenda ‘mume wangu’...

T L