• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Karen Nyamu: Ninaomba Mungu abadili ajenda ‘mume wangu’ Samidoh na Edday warudiane 

Karen Nyamu: Ninaomba Mungu abadili ajenda ‘mume wangu’ Samidoh na Edday warudiane 

NA SAMMY WAWERU

SENETA maalum Karen Nyamu amesema ombi lake limekuwa ni kuona ‘mumewe’ Samuel Muchoki almaarufu ‘Samidoh’ na Edday Nderitu wanarudiana.

Dalili zote zinaonyesha mwanamuziki Samidoh ametemwa na Edday, hasa baada ya kuwa ‘baby daddy’ na Karen.

Kupitia video aliyopeperusha mbashara mitandaoni, Karen anasema amekuwa akiomba Mungu arejeshe pamoja wanandoa hao.

“Mimi kuna vile nimekuwa nikiomba; Mungu ulinipa watoto warembo, baba yao (akimaanisha Samidoh) anawapenda sana. Ana watoto na mwanamke mwingine, anaowapenda sana. Niliambia Mungu achukue usukani wa mambo,” Karen alielezea.

Samidoh na Edday wana watoto watatu, ila ndoa yao iliingia doa baada ya msanii huyo wa nyimbo za Mugithi kuenda nje ya ndoa.

Aidha, Samidoh na Karen wamejaliwa watoto wawili mapenzi yao yakionekana kunoga na kupamba moto.

Edday, hata hivyo, Mei 1, 2023 alisafiri ng’ambo, Amerika, katika kile kilionekana kama kusaka amani ya majeraha ya moyo.

Kwa sasa, anaishi na bintiamu wa Samidoh, Bernice Saroni.

Edday tayari ametangaza kumtema Samidoh, akisisitiza kwamba hatastahimili ndoa yenye zaidi ya mke mmoja.

Mapema 2023, alitoa tahadhari hata kabla ya kuachana na Samidoh na kusafiri Amerika.

Isitoshe, wanawe mwanamuziki huyo wa kibao tajika ‘Kairitu Gakwa’ – Binti yangu, wamejiunga na shule Amerika.

Kulingana na Karen, amekuwa akimlilia Mungu kwa sababu ya Edday.

“Tunatarajia mema, wataelewana. Hatujakata tamaa na huo upande mwingine (akiashiria Edday),” akaelezea, akijibu maswali ya wafuasi wake waliomkashifu kwa kuvunja ndoa ya wenyewe.

Seneta huyo alijitetea akisema “Mimi sikuvunja ndoa ya yeyote, ni mume Mungu aliniletea na kunijalia”.

Alisikika kujutia kuchangia Samidoh kutemwa na mke wake.

“Licha ya kuwa ninahisi vizuri, watoto wangu wana baba anayewapenda na nina mwanamume ninayempenda. Sisikii vizuri kuona ule upande mwingine hauna furaha”.

Desemba 2022, Karen alivamia kilabu kimoja Dubai ambapo Samidoh alikuwa akitumbuiza mashabiki wake.

Alikuwa ameandamana na mkewe Edday na alilazimika kumuondoa dhidi ya drama iliyoibuka.

Karen, ameweka wazi mitandaoni uhusiano wake na Samidoh.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yazindua awamu ya pili ya usajili kwa mpango wa...

Wanamazingira waingiwa na wasiwasi mikoko ikifa Kitangani

T L