• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Shamrashamra: Usalama waimarishwa wageni wakifurika Pwani

Shamrashamra: Usalama waimarishwa wageni wakifurika Pwani

NA SIAGO CECE

USALAMA umeimarishwa katika barabara kuu za Pwani huku watalii wa ndani na wa kigeni wakifurika kwa msimu huu wa sherehe za sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Polisi wanafanya ukaguzi wa vitambulisho mara kwa mara kwenye barabara kuu kadha, ili kuthibitisha uraia wa abiria katika magari ya umma.

Katika Kaunti ya Kwale, vizuizi vya barabarani vimewekwa Kombani, Matuga na Ramisi ambapo abiria wanatakiwa kutoa vitambulisho vyao kabla kuendelea na safari.

“Tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kutambua wageni wasio raia ambao wanaweza kutumia msimu huu wa makaribisho ya watalii kupenyeza maeneo mengine ya nchi,” alisema Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kwale, Stephen Ng’etich.

Bw Ng’etich alihoji kuwa kutokana kwamba Kwale ni kaunti inayopakana na mataifa mengine jirani, iko hatarini zaidi kupokea raia wa kigeni kupitia mipaka iliyo wazi.

Kuimarisha doria, kamanda huyo alisema polisi ndio watasimamia barabara kuu kama vile Likoni-Lungalunga na Mombasa-Nairobi ili kuhakikisha magari yanadhibiti mwendo inavyotakiwa na hivyo kupunguza visa vya ajali.

Pia alisema hoteli zimeagizwa kuhifadhi orodha ya majina ya wageni wote wanaoingia na kutoka humo.

“Hatutaki maadui wawe karibu nasi,” Bw Ng’etich alisema na kuongeza kuwa doria zimeongezwa huku maafisa wote wa polisi waliokuwa likizoni wakitakiwa kuwa kazini.

Operesheni hizo zimeratibiwa kuendelea hadi Januari shule zitakapofunguliwa.

Maeneo mengine ambako ulinzi umeimarishwa ni mjini, maabadi na sehemu za starehe na burudani.

Wakati huo huo, Bw Ng’etich alitaka wanaosafiri kwenda maeneo mengine kuwafahamisha majirani na polisi kuhusu wanapoishi, ili kuzuia majambazi kuvunja nyumba zao wakati huo ambao hawatakuwepo.

Katika kivuko cha Likoni, msongamano umeanza kushuhudiwa huku maelfu ya wakazi na pia magari yakisafiri kati ya Mombasa na Kwale.

Idadi ya watu katika eneo la Pwani imeongezeka huku watalii wakizuru eneo hilo. PICHA | SIAGO CECE

Haya yanajiri huku wakazi wa Kwale wakisihi polisi kuongeza doria zao kwenye fuo za Bahari Hindi wakisema zimegeuka maficho ya wahalifu na wakosa maadili.

“Kuna vituko vingi vinaendelezwa na vijana baharini. Wanajificha maeneo hayo kwa sababu ni nadra polisi kuwapata,” alihoji mkazi wa Msambweni, Hassan Swaleh.

Bw Swaleh alihimiza wazazi kuhakikisha wanafuatilia watoto wao wakati huu wako nyumbani kwa likizo ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vya uhalifu.

Wakati huo huo, biashara tayari imeanza kunoga katika sekta ya utalii wadau wakisema msimu huu wa Krismasi ndio bora zaidi tangu janga la Covid-19, watalii wa ndani na kigeni wakitembelea vivutio mbalimbali.

Meneja Mkuu wa hoteli ya Jacaranda Indian Ocean Beach Resort, Duncan Kiroro, alisema kwa sasa wamepata wageni asilimia 80 huku wengi zaidi wakitarajiwa kuhifadhi vyumba ifikapo wiki ijayo.

“Hatuwezi kulalamika mwaka huu, tumepokea wageni wengi sana kutoka ndani na nje ya nchi. Tayari wengi wamehifadhi hadi mwanzo wa mwaka,” alieleza Bw Kiroro.

Aliongeza kuwa usafiri wa treni zinazotumia reli ya SGR umesaidia Wakenya wengi kutoka sehemu za bara kuzuru mji wa kitalii wa Diani.

  • Tags

You can share this post!

Simbajike Wamuchomba akataa kuunga ripoti ya kumtengenezea...

Mshukiwa wa wizi wa pesa kutoka kwa maajenti wa M-Pesa...

T L