• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Shemeji wa Mzee Moi ang’ang’ania kupata umiliki wa kipande cha shamba cha rais huyo mstaafu

Shemeji wa Mzee Moi ang’ang’ania kupata umiliki wa kipande cha shamba cha rais huyo mstaafu

NA TITUS OMINDE

SHEMEJI wa Rais mstaafu marehemu Daniel Arap Moi amepinga uamuzi wa mahakama ambapo alipoteza ekari 51 za ardhi kwa familia ya Mzee Moi.

Bi Emily Chesang mwenye umri wa miaka 74, binamu wa marehemu Lena Moi, mke wa marehemu rais, amepinga uamuzi wa Mahakama ya Ardhi na Mazingira mjini Eldoret baada ya kupoteza kipande hicho cha shamba kwa familia ya Moi.

Shamba hilo liko eneo la Mumberes, Kaunti Ndogo ya Koibatek.

Bi Chesang anadai kuwa alipewa shamba hilo na binamu yake kama zawadi baada ya kumuuguza alipokuwa mgonjwa.

Katika hati yake ya kiapo ya kupinga uamuzi wa familia ya Moi, Bi Chesang alidai kuwa uamuzi huo ulitupilia mbali ushahidi wake ambapo nyaraka zake nyingi zilikosekana katika faili yake na hivyo kudhoofisha utetezi wake.

Pia anadai kuwa ukosefu wake kupata habari kuhusu mchakato wa mahakama uliathiri vibaya kesi yake.

“Sikupewa nafasi ya kufika mahakamani kujitetea kama mshtakiwa. Uamuzi huo ulifanywa kwa haraka ambapo suala hilo lilihamishiwa Eldoret badala ya Nakuru bila idhini yangu,” Bi Chesang alisema.

Chesang ana imani kwamba akipewa nafasi atathibitishia mahakama kwamba ana haki ya kumiliki ardhi hiyo yenye utata.

Kulingana na Bi Chesang, uamuzi huo haukuchangia utetezi wake kwani aliachwa gizani wakati wa shughuli nzima ya mahakama.

Alifukuzwa kutoka shamba hilo mnamo 2020 baada ya uamuzi wa korti.

“Familia yangu imeachwa ikirandaranda mitaani, nimepoteza kila kitu nilichokuwa nacho, watoto wangu wametawanywa. Natoa wito kwa wataalamu wa sheria kunisaidia kurejeshewa ardhi yangu,” alisema.

Pia anadai kuwa kampuni moja ya udalali Nakuru inayodaiwa kukodiwa na familia ya Mzee Moi inamtishia kwa kutaka alipwe gharama ya kesi hiyo lakini akapewa fursa ya kukata rufaa dhidi ya kesi hiyo katika mahakama ya rufaa.

Akitoa uamuzi huo uliopendelea ardhi na mazingira ya familia ya Moi Jaji, Jaji E.Oboga alithibitisha kwamba Bi Chesang alikaa shambani humo kuanzia Januari 1995 hadi kifo cha Lena Moi mnamo 2004.

Mahakama ilisema kwamba kwa kuwa mlalamishi alikaa katika shamba lililozozaniwa kwa idhini ya Lena Moi, hawezi kudai kuwa mmiliki wa ardhi hiyo.

Kulingana na mahakama, Jonathan Moi alisajiliwa kuwa mmiliki wa ardhi hiyo mnamo Juni 8, 2007 kabla ya kuihamishia kwa bintiye Barbara Chebet Moi mnamo Oktoba 2010.

Chesang aliombwa kuondoka katika eneo hilo mwaka wa 2017 alipojaribu kumzika mjukuu wake katika shamba hilo.

Mahakama ilibaini kuwa kutokana na kipindi ambacho Bi Chesang alikaa katika shamba hilo baada ya Jonathan Moi kuwa mmiliki aliyesajiliwa, hawezi kudai umiliki kutokana na muda mfupi aliokaa katika shamba hilo.

Kulingana na matokeo ya mahakama, muda ambao Bi Chesang alikaa katika ardhi husika ulikuwa mfupi.

Kisheria, mtu anapaswa kudai umiliki wa ardhi baada ya ‘kuikalia’ muda wa miaka 12.

“Kutokana na muda mfupi mlalamishi alikuwa akiishi katika ardhi hiyo, ni wazi kwamba hakuwa na sababu tosha za kudai umiliki wa shamba hilo.

“Kwa hivyo naona kuwa kesi yake haina mashiko. Hivyo basi imetupiliwa mbali na gharama kwa mlalamishi,” aliamua Jaji E.Obaga wa Mahakama ya Ardhi na Mazingira ya Eldoret.

 

  • Tags

You can share this post!

Barabara: Kilomita 21,556 za lami tangu Kenya kuwa huru

AMINI USIAMINI: ‘Bullet ant’ akiuma sehemu...

T L