• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Sitakuangusha, Mudavadi amuahidi Rais Ruto

Sitakuangusha, Mudavadi amuahidi Rais Ruto

NA CHARLES WASONGA

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi amemshukuru Rais William Ruto kwa kumwongeza majukumu zaidi yenye hadhi kubwa katika mabadiliko aliyofanya katika baraza lake la mawaziri.

Kwenye ujumbe aliouweka katika akaunti yake ya mtandao wa X (zamani Twitter), Bw Mudavadi pia alimpongeza Dkt Ruto kwa “kuweka imani yake kwangu na kuniongezea majukumu zaidi ya kusimamia Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Masuala ya Wakenya wanaoishi ughaibuni”.

“Ninafahamu vyema umuhimu wa wajibu huu mkubwa na ninakumbatia nafasi hii kwa ahadi kuwa nitafanya kazi kwa bidii na kujitolea,” Bw Mudavadi akasema.

“Naahidi kuendelea kuwahudumia Wakenya na nchi yetu kwa moyo wa kujitolea, uadilifu na bidii. Na nitafuatilia, kuendeleza na kulinda masilahi ya Wakenya ndani na nje ya mipaka yetu. PAMOJA TUDUMISHE HADHI YA KENYA NDANI NA NJE YA MIPAKA YETU,” akaongeza.

Bw Mudavadi ambaye alionekana kuvuna pakubwa katika mabadiliko ambayo Rais Ruto alifanya serikalini mnamo Jumatano, Oktoba 4, 2023, usiku, sasa atakuwa akitekeleza majukumu ambayo yalitekelezwa zamani na Dkt Alfred Mutua.

Dkt Mutua sasa amehamishwa hadi katika Wizara ya Utalii na Wanyamapori. Naye Bi Peninah Malonza ambaye alikuwa akishikilia wizara hiyo amehamishwa hadi kwa Wizara ya Afrika Mashariki na Maeneo Kame (Asal).

Kupandishwa hadhi kwa Mudavadi kumechangamsha ngome yake ya kisiasa katika eneo la Magharibi mwa Kenya huku wadadisi wakisema kuwa hatua hiyo inalenga kumdhibiti Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Lakini katika serikali ya Kenya Kwanza, Bw Mudavadi ndiye wa tatu kimamlaka nyuma ya Bw Gachagua na Rais Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu yakabidhiwa maktaba ya...

GWIJI WA WIKI: Dkt Alexander Rotich

T L