• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
TSC yafuta walimu 43 kwa ukosefu wa maadili

TSC yafuta walimu 43 kwa ukosefu wa maadili

Na WANDERI KANAU

TUME ya Kuwaajiri Walimu (TSC) imewafuta kazi walimu 43 kwa tuhuma za “kukiuka kanuni na maadili ya taaluma ya ualimu.”

Ingawa tume haikueleza wazi sababu maalum za kuwachukulia hatua hiyo, ripoti iliyotoa majuzi ilionyesha kwamba wengi wanahusishwa na makosa ya kuwadhulumu kimapenzi wanafunzi wao.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali jana Ijumaa, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bi Nancy Macharia, alisema tume haitasita kumchukulia hatua mwalimu yeyote atakayehusishwa na tuhuma za kutowajibika.

“Kama tume, wajibu wetu ni kuhakikisha walimu wanaendesha majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia kanuni za ualimu ifaavyo,” akasema Bi Macharia.

Alisema walimu hao hawapaswi kuajiriwa katika taasisi yoyote ya elimu.

“Mwalimu atakayepatikana akifunza atapigwa faini ya Sh100,000, kufungwa kifungo cha miaka miwili gerezani au kukabiliwa na adhabu zote mbili,” akasema Bi Macharia kwenye taarifa.

Mwaka 2020, tume iliwafuta kazi walimu 30 kwa makosa mbalimbali, kiwango kikubwa kikiwa vitendo vinavyohusiana na mahusiano ya kimapenzi baina yao na wanafunzi.

Katika kuchukua hatua hiyo, tume ilisema ilikuwa na ushahidi wa kutosha kudhihirisha makosa yao.

Mnamo 2019, tume iliwafuta kazi walimu 42 kwa kukosa kuhudhuria mafunzo maalum kuhusu Mfumo Mpya wa Elimu (CBC).

Walimu hao pia walilaumiwa kwa kuvuruga mafunzo yaliyokuwa yakiendelea katika vituo mbalimbali.

Tume vile vile ilitangaza kuwapa likizo ya lazima walimu 124 huku wengine 30 wakipata barua za kuwaonya.

Kijumla, walimu 219 kutoka maeneo ya Kakamega, Bungoma, Kajiado, Kitui, Machakos, Garissa, Kisii, Nyamira, Vihiga na Kwale waliadhibiwa kutokana na makosa tofauti yanayohusiana na kutoshiriki kwenye mafunzo hayo.

Kulingana na ripoti ya TSC, kaunti zilizoathiriwa zaidi ni zile zilizo katika maeneo kame.

Kaunti hizo ni kama Mandera, Narok, Kajiado, Turkana, Samburu kati ya zingine.

Mwezi uliopita, walimu watatu katika Kaunti ya Narok walifutwa kazi na tume hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kuwaona wanafunzi wasichana wa shule ya msingi, licha ya kuwa chini ya umri wa miaka 18.

Kulingana na ripoti iliyotolewa majuzi na shirika la utafiti la Twaweza, wasichana wengi katika maeneo kame hulazimika kushiriki ngono wanaume waliowazidi umri kutokana na hali za umaskini katika familia zao.

“Wakati msichana anapojipata katika mazingira ya umaskini, huwa hana uamuzi mwingine ila kukubali vishawishi vya wanaume. Hili huwawezesha kujikimu kimaisha kwa kununua bidhaa za kimsingi kama sodo,” ikaeleza ripoti hiyo.

Ripoti ilisema ni lazima serikali iwekeze fedha nyingi katika kuwasaidia wasichana kupata bidhaa hizo, ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao bila vikwazo vyovyote.

Kwa mujibu wa Bi Muthoni Ouko, ambaye ni mwanaharakati kuhusu masuala ya elimu, wakati umefika taasisi husika za elimu kuanzisha juhudi kuwahamasisha wanafunzi kuhusu athari za kujihusisha katika mahusiano ya kimapenzi na walimu wao.

Alisema hatua hiyo huenda ikawazindua wanafunzi na kupunguza visa hivyo, kwani vinaendelea kuongezeka.

“Kwa kuchukua mkakati huo, kuna uwezekano mkubwa visa hivyo kupungua,” akasema.

You can share this post!

KAMAU: Wakati umewadia Miguna aruhusiwe kurejea Kenya

Ruto aahirisha kikao cha wawaniaji wa Bonde la Ufa

T L