• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:50 AM
KAMAU: Wakati umewadia Miguna aruhusiwe kurejea Kenya

KAMAU: Wakati umewadia Miguna aruhusiwe kurejea Kenya

Na WANDERI KAMAU

SIMULIZI za mashujaa walioshiriki katika harakati za ukombozi nchini huwa chungu.

Wakati mwingine, huwa zinaatua moyo.

Ni simulizi zinazoonyesha ukatili ambao serikali ya kikoloni ilikuwa ikiwafanyia Waafrika walioonekana kupinga utawala wake.

Ukatili mwingine ambao utawala huo uliwafanyia Waafrika ni kuwapeleka vizuizini uhamishoni.

Kwa mfano, wanaharakati kama Harry Thuku walipelekwa kizuizini mjini Kismayu, nchini Somalia.

Thuku alikuwa miongoni mwa kizazi cha kwanza cha Waafrika waliojitokeza kupinga hatua ya Waingereza kuvamia mashamba ya Wakenya katika miaka ya ishirini na thelathini.

Bila shaka, Wazungu walikuwa huru kufanya hivyo, kwani hawakumwogopa yeyote.Kando na Thuku, Shujaa Kung’u Karumba pia anadaiwa kutojulikana alikotowekea, baada ya kuripotiwa kuelekea nchini Uganda miaka michache kabla ya Kenya kujipatia uhuru.

Wakati huo, vitendo vya Wazungu vilieleweka.Walikuwa huru kuwahangaisha Waafrika kwa namna yoyote waliyotaka.

Hata hivyo, inasikitisha wakati Mwafrika anapomhamisha mwenzake kutoka nchi yake au hata kumzuia kurudi huko.Ndiyo taswira inayoandama masaibu yanayomkumba wakili Miguna Miguna, ambaye amekuwa uhamishoni nchini Canada tangu Februari 2018.

Tangu wakati huo, juhudi za Dkt Miguna kurudi nchini zimekuwa zikigonga mwamba.

Kwenye juhudi hizo, serikali imekuwa ikitoa kila aina ya kisingizio kumzuia kurejea.

Ni hatua ambayo imemfanya aliyekuwa Jaji Mkuu, Dkt Willy Mutunga, kusema kwamba yuko tayari kuandamana na Dkt Miguna anapopanga kurejea nchini mnamo Novemba.

Kimantiki, ni makosa kwa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuendelea kumhangaisha Dkt Miguna ilhali washabuni mwafaka wa kisiasa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Kulingana na serikali, sababu kuu ya “kumrejesha” Dkt Miguna nchini Canada ilitokana na hatua yake kumwapisha Bw Odinga kama “Rais wa Wananchi” mnamo Januari 30, 2018.

Hilo lilifuatia utata uliokumba uchaguzi mkuu wa urais wa 2017, ambapo Bw Odinga alisusia kushiriki.

Kwa sasa, sidhani kuna sababu yoyote maalum kwa serikali kumzuia Dkt Miguna kurejea nchini.

Kwanza, yeye si tishio la usalama wa taifa, kama ilivyodaiwa.

Pili, wakili huyo ni raia wa Kenya. Mbona anazuiwa kurejea Kenya?

Wakati umefika kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga kuonyesha kuwa maafikiano yao ya kisiasa hayapo kwa maneno tu, bali kwa vitendo.

Ni wakati Bw Odinga akumbuke alivyohisi wakati alikuwa gerezani, hadi akakosa kuhudhuria mazishi ya mamake.

Kama mtu anayejua uchungu wa kuwakosa jamaa wa karibu, ni wakati atumie ushawishi wake kumwezesha Dkt Miguna kurejea nchini na kutangamana tena na jamaa zake.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Nairobi kupata gavana mpya baada ya kutimuliwa kwa Sonko

TSC yafuta walimu 43 kwa ukosefu wa maadili

T L