• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Vitisho vyachacha kati ya Azimio na Kenya Kwanza

Vitisho vyachacha kati ya Azimio na Kenya Kwanza

WANDERI KAMAU Na BENSON MATHEKA

MAZUNGUMZO ya maridhiano yanayotarajiwa kati ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja One Kenya yametawaliwa na vitisho hata kabla ya kuanza.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuanza wiki hii huku pande hizo mbili zikirushiana vitisho.

Vitisho hivyo vinawahusisha Rais William Ruto na washirika wake kwa upande mmoja na kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga na washirika wake kwa upande mwingine.

Mnamo Jumamosi, Rais Ruto alisisitiza kuwa hatakubali handisheki yoyote na Raila Odinga.

“Hawa watu waliwasukuma (marais) Daniel Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta na wakapata handisheki. Wanajaribu kunifanyia hivyo, lakini hawatapata hata nusu ya serikali. Hakutakuwepo na handisheki,” akasema Rais Ruto, alipohutubu katika Kaunti ya Kirinyaga.

Dkt Ruto alisisitiza kuwa ataukalia ngumu upinzani, ikiwa utajaribu kuandaa maandamano tena, akisema yamesababisha maafa mengi na uharibifu wa mali.

“Kenya ni taifa linaloongozwa na sheria. Hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuharibu mali ya umma ama ya kibinafsi,” akaongeza Dkt Ruto.Kauli hiyo ilijiri huku Bw Odinga akisisitiza kuwa atatoa mwelekeo mpya kwa wafuasi wake ifikapo Septemba 1, ikiwa mazungumzo hayo hayatakuwa yamekamilika kufikia Agosti 31.

Akihutubu Jumamosi katika eneo la Gem, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alisema kuwa wako tayari kurejelea maandamano ikiwa mazungumzo hayo “hayatazaa matunda yoyote”.

“Kama wana-Azimio, tuko tayari kushiriki kwenye mazungumzo. Tunawapa wale jamaa (Kenya Kwanza) muda wa siku thelathini. Ikiwa huyo jamaa (Ruto) atakaa ngumu, nitatoa amri nyingine,” akasema Bw Odinga.

“Hawatatutisha tukubali masharti yao. Kila upande una masharti na iwapo mazungumzo yatafeli, tutarudi barabarani,” akasema.

Akaongeza: “Tunaenda mezani bila masharti ila wao vile vile wasitoe masharti kwetu. Lakini wasipokuwa tayari kuongea na kukubaliana na sisi, tutachukua hatua tofauti baada ya siku 30.”

Kwenye ziara ya Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya, washirika wake wa karibu walisisitiza kauli yake, kuwa hawatakubali handisheki yoyote baina yake na Bw Odinga.

Kiongozi wa nchi pia ametishia kuzima maandamano yoyote siku za usoni licha ya Azimio kutishia kushtaki polisi wanaotumia nguvu kuyazima katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Bw Odinga alidai kwamba kwa kusifu maafisa wa polisi walioua wafuasi wa upinzani, Rais Ruto alisherehekea vifo vya waliouawa hata bila kuandamana.

“Wakazi wa Mlima Kenya walimchagua Rais Ruto kuwa kiongozi wao. Walikupigia kura wote. Wamesema kwa sauti moja kwamba hawataki handisheki,” akasema Naibu Rais Rigathi Gachagua, alipohutubu katika eneo la Githurai 45, Kaunti ya Kiambu.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu): “Hakuna handisheki. Badala yake, tunataka mazungumzo yazimwe.”

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wa vile vile aliwaunga mkono Bw Gachagua na Bw Nyoro.

“Wakenya wamesema ‘La’ kwa handisheki. Wakenya wanajua kile tutakuwa tukijadili katika hoteli ya Serena. Nitakuwa katika mazungumzo ya Obasanjo kupinga wazo lolote linalohusu handisheki,” akasema Bw Ichung’wa.

Hapo jana, washirika wa Bw Odinga walijitokeza kumtetea vikali, wakionekana kuwajibu washirika wa Rais Ruto.

Kwenye ibada ya kanisa katika eneobunge la Embakasi Magharibi, Kaunti ya Nairobi jana, viongozi hao walisema hawatakubali vitisho kutoka kwa Kenya Kwanza hata kidogo.

“Kututisha hakutawasaidia watu katika siku za baadaye. Hatutaki handisheki. Punguza gharama ya maisha na hutaona nikikukabili kila mara,” akasema Seneta Edwin Sifuna.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa naye alisema: “Rais Ruto ndiye aliyeitisha mazungumzo haya. Tunataka kuweka wazi kwamba hatutaki handisheki.”

Kauli kama hiyo ilitolewa na Seneta Enoch Wambua (Kitui): “Hatutatishika hata kidogo kwenye shinikizo zetu. Kuna wale wanaodai kuwa tunataka handisheki, lakini hilo si kweli. Hakuna yeyote mwenye mamlaka ya kutuzuia kutekeleza haki yetu.”

Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema lengo na jukumu lao ni kuwatetea Wakenya.

Alisema hali nchini imekuwa mbaya kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha. Aliongeza kuwa licha ya vitisho hivyo, watasimama kidete, na hawatakubali kutishwa na yeyote.

Macho yote ya Wakenya sasa yako kwa mirengo hiyo miwili, kuhusu vile itaendesha mazungumzo ya maridhiano.

 

  • Tags

You can share this post!

Hofu ajira kupotea SGR ikifika Uganda

WANTO WARUI: Haifai kuweka shule za chekechea pamoja na...

T L