• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:55 AM
Wakenya wasukumwa kona mbaya, bei ya gesi ya kupikia ikipanda tena

Wakenya wasukumwa kona mbaya, bei ya gesi ya kupikia ikipanda tena

NA CHARLES WASONGA

WAKENYA, kwa mara nyingine, watalazimika kulipa Sh500 zaidi kujaza mtungi wa gesi wa kilo sita baada ya bei ya bidhaa hiyo kupanda tena licha ya kushuka hadi chini ya Sh1,000 mwezi jana.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa wauzaji wa rejareja katika maeneo ya Nairobi na Nakuru  wameongeza bei ya kilo sita kutoka Sh950 hadi Sh1,400.

Katika maeneo haya, mtungi wa kilo tatu unajazwa kwa Sh650 (kutoka bei ya Sh500 mwezi Agosti) huku ule wa kilo 13 ukigharimu Sh3,200 kutoka Sh2,500 mwezi huo.

Mfanyabiashara mmoja alisema kuwa kupanda kwa bei ya gesi kumechangiwa na ongezeko la bei ya mafuta, kwa kiwango cha juu, katika mwezi wa Septemba.

“Bei ya gesi inahusishwa na bei ya mafuta. Kwa hivyo, bei ya mafuta ikipanda, bei ya gesi pia huongezeka. Mwezi Agosti, bei ya mtungi wa kilo sita ilishuka hadi Sh950, lakini sasa bei imepanda hadi kati ya Sh1,300 na Sh1,400,” akasema mfanyabiashara huyo aliyeomba tulibane jina lake.

Kuongezwa kwa bei ya gesi ya kupikia kutawaumiza zaidi Wakenya ambao tayari wanazongwa na gharama ya juu ya chakula, umeme na nauli, kupandishwa kwa bei ya mafuta kuanzia Septemba 15, 2023.

Ni wiki jana tu, ambapo Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) ilitangaza kuwa bei ya stima itapanda kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta na kudorora kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhdi ya sarafu za kigeni, haswa dola ya Amerika.

Bei ya gesi inapanda wakati ambapo bei ya mafuta ya taa ambayo hutumiwa na watu wa mapato ya chini pia imepanda hadi Sh133.09 kwa lita jijini Nairobi.

Mnamo Agosti, bei ya gesi ilishuhuka baada ya serikali kuondoa ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa bidhaa hiyo ili kuendeleza matumizi ya kawi safi.

Aidha, baraza la mawaziri limeidhinisha pendekezo la kupunguzwa kwa aina zingine za ushuru zinazotozwa gesi ya kupikia, ili kufanikisha ajenda yake kuhusu matumizi ya kawi isiyochafua mazingira.

  • Tags

You can share this post!

Wataalam waonya kuhusu athari za tabianchi kwa kilimo na...

Sakaja avuruga kadi za Gachagua 2032

T L