• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Wataalam waonya kuhusu athari za tabianchi kwa kilimo na ufugaji

Wataalam waonya kuhusu athari za tabianchi kwa kilimo na ufugaji

NA PAULINE ONGAJI

KWA Bi Evelyn Maison, 37, mfugaji wa nyuki eneo la Laikipia, mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kwa shughuli yake na kuathiri kiwango cha asali anayovuna.

Bi Maison ni mmoja wa wanachama wa kikundi cha wanawake cha Ethi-Il ngwesi Women group, ambacho kilianzisha shughuli hii miaka miwili iliyopita, kama mbinu ya kupata kipato. Lakini katika siku za hivi majuzi, kumekuwa na mabadiliko ambayo yameathiri idadi ya nyuki walio nao, na hivyo kupunguza kiwango cha asali wanayovuna.

“Tumekuwa tukikumbwa na tatizo la ukame ambao umeathiri hasa vyanzo vya vyakula, na hivyo kusababisha nyuki kahama, na hata waliosalia kuwa katika hatari ya kuangamia. Tuna wasiwasi kuhusu siku zijazo kwani kiwango cha asali wanayopata kimekuwa kikipungua,” aeleza.

Bi Maison ni mmoja wa wakulima ambao wataendelea kuathirika pakubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameendelea kushuhudiwa hapa barani.

Kulingana na wataalam, licha ya kwamba Afrika inachangia asilimia 4 pekee ya uzalishaji wa gesi zinazosababisha ongezeko la joto ulimwenguni (greenhouse gases GHG), katika siku zijazo, bara hili litaendelea kukabiliwa na majanga yanayochochewa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Jopo la mataifa tofauti kuhusu mabadiliko la tabianchi IPCC, linasema kwamba viwango vya halijoto barani vinatabiriwa kuongezeka ikilinganishwa na mahali pengine popote duniani, huku ongezeko hili likitarajiwa kuwa kati ya 0.2? na 0.5?.

Hapa nchini Kenya, ripoti ya mwaka wa 2020 ya Idara ya utabiri wa hali ya anga KMD kuhusu hali ya tabianchi, ilionyesha kwamba viwango vya joto vilivyonakiliwa mwaka wa 2020 vilikuwa vya juu zaidi vikilinganishwa na viwango wastani vilivyorekodiwa kati ya mwaka wa 1981 na 2012, na msimu wa baridi wa Kenya (Juni hadi Agosti) ulinakili mabadiliko makubwa zaidi yakilinganishwa na viwango vya kawaida ikilinganishwa na miezi mingine mwaka huo.

Katika eneo la Afrika Mashariki, wanasayansi wamekuwa wakitoa onyo kuhusu ongezeko la viwango vya joto na vipindi vya ukame.

Ni jambo ambalo lilishuhudiwa katika upembe wa Afrika ambapo eneo hili lilikumbwa na ukame mbaya kuwahi ushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40, ambapo takriban watu 43,000 nchini Somalia walifariki mwaka 2022.

Athari za ukame ulioshuhudiwa zinatarajiwa kuathiri sekta ya kilimo katika eneo hili, na hivyo kuathiri mifumo ya chakula ambayo tayari ni dhaifu. Baadhi ya athari ni pamoja na kupungua kwa mazao ya kilimo.

Kuna sababu nyingi zinazofanya mabadiliko ya tabianchi kuathiri sekta ya kilimo barani Afrika. Takriban asilimia 95 ya wakulima barani hawana mifumo ya unyunyizaji mashamba maji, kumaanisha kwamba wanategemea mvua.

“Mabadiliko ya tabianchi ni tishio zaidi kwa kilimo barani Afrika kwa sababu kinategemea sana hali ya anga,” aeleza Dkt Sheila Ochugboju, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kutoa taarifa za kisayansi la Alliance for Science.

Wanasayansi wanatabiri kupungua kwa viwango vya mvua katika maeneo tofauti barani, na vipindi vya ukame vinaendela kuongeza.

Hii inamaanisha kwamba wakulima wanaoishi katika maeneo kame barani watakumbwa na matatizo zaidi ya kufikia maji ya kunyunyizia mashamba yao. Kulingana na wataalam, mimea inayoliwa barani kwa wingi kama vile mahindi na ngano itakumbwa na ugumu wa kuota katika mazingira haya.

Inasemekana kwamba endapo viwango vya halijoto vitaongongezeka kwa nyusi 2?, ukuzaji wa mimea katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara utapungua kwa asilimia 10. Ikiwa viwango vya joto vitazidi nyusi 2? mazao ya mimea hii itapungua kwa asilimia 20, na ikiwa mambo yatakuwa mabaya zaidi na viwango vya halijoto viongezeke kwa nyusi 3?, basi maeneo yanayojulikana kwa ukuzaji wa mimea kama vile mahindi na mtama barani Afrika, hayatahimili kilimo hiki.

Hii itaathiri uwezo wa mataifa ya Afrika, Kenya miongoni mwao, kujitosheleza kivyakula.

Na tayari athari hizi zimeanza kushuhudiwa hapa nchini. Ripoti ya mwaka wa 2021 ya kutathmini viwango vya njaa (Global Hunger Index Report) inaonyesha kwamba Kenya ingali inakumbwa na tatizo la baa la njaa huku ikiorodheshwa ya 87 miongoni mwa nchi 116.

Mabadiliko ya tabianchi pia yana athari kwa ufugaji. Ongezeko la viwango vya halijoto vinapunguza uzalishaji wa mifugo, vile vile kukua kwa mimea inayotoa lishe ya mifugo. Katika maeneo ya ufugaji kama vile Kaskazini Mashariki mwa Kenya, Idara ya Mifugo nchini ilithibitisha kwamba zaidi ya mifugo 2.5 waliangamia kutokana na ukame.

Kulingana na Dkt Todd Crane, Mkuu wa wajumbe na mwanasayansi mkuu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mifugo ILRI, mabadiliko haya yanatarajiwa kuathiri malisho ya wanyama.

“Mabadiliko ya tabinchi yanaongeza majanga ya kimazingira kama vile ukame, suala linaloathiri ukuzaji wa mimea inayotoa lishe ya wanyama, kumaanisha kwamba wafugaji watakuwa na matatizo ya kulisha wanyama wao,” aongeza.

Hii ni hatari hasa kwa jamii za maeneo ya ufugaji ambazo kwa miaka zimekuwa zikitegemea mifugo. Aidha, kuathirika kwa sekta ya ufugaji kutaathiri utoshelevu wa chakula nchini.

Kwa hivyo, huku changamoto zikiendelea kuikumba sekta ya kilimo, ili kuijiandaa kwa changamoto siku za usoni, wataalam wanasema kwamba sharti mifumo ya vyakula barani iimarike.

Kulingana na Bw Bernard Kimoro, Mkuu wa kitengo cha mabadiliko ya tabianchi na mbinu bora za ufugaji katika Idara ya kitaifa ya ustawi wa mifugo, kuna haja ya kuwekeza katika mbinu za kisasa za kilimo.

“Mojawapo ya njia za kufanya hivyo ni kukumbatia teknolojia katika mifumo ya vyakula ili kuzalisha mimea inayoweza stahimili ukame na magonjwa, vile vile ongezeko la viwango vya chumvi kwenye udongo,” aeleza Dkt Ochugboju.

  • Tags

You can share this post!

Polisi watano wakamatwa na maafisa wa EACC kwa kuitisha...

Wakenya wasukumwa kona mbaya, bei ya gesi ya kupikia...

T L