• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Watu 66 waliookolewa Shakahola kusota jela Krismasi

Watu 66 waliookolewa Shakahola kusota jela Krismasi

NA BRIAN OCHARO

WATU 66 waliookolewa katika msitu wa Shakahola watasota jela Krismasi na Mwaka Mpya baada ya mahakama kuipa serikali siku nyingine 130 kuamua ikiwa inakusudia kuwafungulia mashtaka au kuwachukulia kama mashahidi.

Hakimu Mwandamizi Mkuu wa Shanzu Joe Omido alisema alishawishiwa kuwa serikali ilihitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi wake.

“Ni maoni yangu kuwa muda mfupi kuliko makadirio ya siku 160 utatosha. Nitawaruhusu washtakiwa kuendelea kukaa rumande kwa siku 130 ambazo naamini zitatimiza malengo yaliyokusudiwa,” alisema hakimu huyo.

Muda wa siku 130 utaanza Septemba 11, 2023, na utaisha Januari 18, 2024.

Mahakama iliambiwa kuwa uchunguzi umebaini kuwa manusura hao wanaweza kuwa wamefanya makosa ya jinai dhidi ya watoto wao, ambao hawajulikani waliko.

“Katika baadhi ya matukio, familia nzima ya msingi kabisa inaweza kuwa imeangamizwa,” Inspekta wa Polisi Raphael Wanjohi alisema.

Uchunguzi huo utajumuisha chembechembe za  DNA kutoka kwa miili 429 iliyofukuliwa hadi sasa.

Afisa huyo pia alisema anahitaji muda wa kutosha kusafiri nchi nzima kuwatafuta na kuwafikia jamaa za marehemu kwa madhumuni ya kufanya uchunguzi na kukusanya sampuli za DNA kwa ajili ya uchunguzi na kulinganisha na wale waliofukuliwa.

“Kwa kuwa kuna miili  ilizikwa bila vibali vya kuzika, ipo haja ya kuwatambua marehemu, jambo ambalo linaleta changamoto kwa kuwa wapelelezi hawana vitambulisho wala nyaraka nyingine za watu waliofariki,” alisema

Mpelelezi alisema mchakato wa utambuzi wa wahasiriwa na shahidi uko katika gia na unahitaji muda wa kutosha kutokana na ugumu wa upelelezi.

Bw Wanjohi aliendelea kusema kwamba polisi wako katika harakati za kuchimba data ya mawasiliano kutoka kwa vifaa vilivyopatikana na miamala ya kifedha kwa nia ya kupata utambulisho wa mamia ya watu waliofariki.

Lakini manusura hao kupitia kwa wakili wao Bw Mureti walipinga ombi hili, wakisema kwamba halijafichua sababu za msingi zinazoweza kulazimiza mahakama kutoa amri ya kuwazuilia zaidi.

“Serikali ina uwezo wa kufanya na kuhitimisha upelelezi wa suala hili bila ulazima wa kuwashikilia washtakiwa,” alisema.

Bw Mureti alisema ikiwa wengi wa waliohojiwa walikataa kurekodi taarifa, walikuwa wakitumia haki zao za kikatiba kunyamaza na hivyo hawawezi kulaumiwa kwa kufanya hivyo.

Alisema zaidi kwamba ripoti ya uchunguzi wa kijamii iliyotayarishwa na kuwasilishwa na ofisi ya afisa wa urekebishaji wa tabia inaonyesha kuwa wengi wa washtakiwa hawawezi kutoroka na kuwa familia zao ziko tayari kuwakubali.

 

Baadhi ya washukiwa 65 waliookolewa kutoka kwa msitu wa Shakahola ulioko Kaunti ya Kilifi, washuka kutoka kwa lori la polisi walipowasili kwa Mahakama ya Shanzu mnamo Juni 12, 2023, kukabiliwa na mashtaka ya kujaribu kujitoa uhai. PICHA | KEVIN ODIT

Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma Jami Yamina alifahamisha mahakama kuwa serikali inawachukulia manusura hao kama washukiwa, akisema kuwa tabia zao zimebadilika na sasa wanachukuliwa kuwa washukiwa katika uchunguzi unaoendelea.

“Tabia zao zimebadilika. Kwa sasa ni washukiwa. Watu wanaoshukiwa kutekeleza uhalifu, ambao wanachunguzwa, hawawezi kuitwa waathiriwa,” akasema Bw Yamina.

Bw Yamina amesema tayari serikali imekusanya ushahidi mwingi dhidi ya manusura hao  hivyo kuna  haja ya kuwaweka gerezani hadi mashtaka yatakapofunguliwa dhidi yao.

“Jinsi uhalifu uliotendwa huko Shakahola kama ilivyoonyeshwa kwenye maombi ya awali ni kwamba masalio ya mwisho ya uhuru wa marehemu yalichukuliwa baada ya vyeti vyao vya kuzaliwa na hata kitambulisha kuharibiwa,” alisema.

Serikali pia imeeleza kuwa ndugu wa marehemu watatakiwa kutoa ushahidi mahakamani mara mshukiwa mkuu Paul Mackenzie na wenzake watakapofunguliwa mashtaka rasmi.

Kesi hiyo itatajwa Januari 18, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Watoto 700 kusherehekea Krismasi, Mwaka Mpya jelani

Serikali yaanza ‘kuvuna’ e-Citizen

T L