• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Watoto 700 kusherehekea Krismasi, Mwaka Mpya jelani

Watoto 700 kusherehekea Krismasi, Mwaka Mpya jelani

NA TITUS OMINDE

WAKATI watoto wengine wakisherehekea Krismasi pamoja na jamaa zao na familia zao, zaidi ya watoto 700 wenye umri wa kati ya siku moja hadi miaka mitano wataadhimisha sikukuu hiyo jelani wakiwa na akina mama zao ambao wanatumikia vifungo au wako rumande wakisubiri mchakato wa kesi zao.

Duniani kote, Wakristo hutumia siku ya Krismasi kuwa ni ya kuleta familia pamoja ambapo wanasherehekea na kuangazia mwaka ulivyokuwa na kujipangia malengo ya Mwaka Mpya.

Lakini sasa kuna watoto wasio na hatia ambao wako gerezani, si kwa sababu wao ni wafungwa, bali kwa sababu ya uhalifu uliofanywa na akina mama zao au walezi wao.

Hakuna jambo la kuhuzunisha zaidi kuliko kuona mpendwa amewekwa rumande wakati dunia nzima inasherehekea Krismasi na Mwaka Mpya.

Miongoni mwa watoto zaidi ya 700 walio katika magereza, 12 kati yao wako katika gereza la wanawake la Eldoret huku wengine wakisambaa katika magereza 18 ya wanawake nchini.

Katibu wa Idara ya Urekebishaji wa Tabia katika Magereza Bi Salome Wairimu Beacco, alisema idara ya magereza inashirikiana na wadau wengine ili kuweka mazingira mazuri kwa watoto kama hao.

Katibu wa Idara ya Urekebishaji wa Tabia katika Magereza Bi Salome Wairimu Beacco alipozuru gereza la Shimo la Tewa jijini Mombasa mnamo Agosti 16, 2023. PICHA | KEVIN ODIT

Bi Beacco alisema kuna mipango ya kuanzisha vituo vya kulelea watoto katika magereza mbalimbali nchini ambavyo vitakuwa vya ubora wa hali ya juu.

Lengo ni kuhakikisha watoto hao wanakua wakiwa katika mazingira shwari.

“Hapa katika gereza la wanawake la Eldoret, tuna watoto 12 ambao waliandamana na akina mama zao. Tunashirikiana na washikadau na washirika wa maendeleo ili tuwe na huduma ya hali ya juu ya kutwa kwa watoto hawa,” alisema Bi Beacco.

Katibu huyo alieleza haja ya kuchunguza njia zote za kisheria ambazo zitasaidia katika kuwaokoa watoto gerezani pamoja na kupunguza msongamano katika magereza yote nchini.

“Tunawashukuru sana washirika wetu wa maendeleo na tunawahimiza wadau wengine kujitokeza na kutusaidia si tu kupunguza msongamano ndani ya magereza lakini pia kuhakikisha wateja wetu wanaishi maisha ya staha kwa kuzingatia ibara ya 28 inayoendana na ibara ya 43 ya Katiba,” aliongeza.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru arusha chambo kwa Mlima Kenya wapende tena Jubilee

Watu 66 waliookolewa Shakahola kusota jela Krismasi

T L