• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Waumini wa kanisa la Good News International walisafirishwa kwa lori la Paul Mackenzie

Waumini wa kanisa la Good News International walisafirishwa kwa lori la Paul Mackenzie

FARHIYA HUSSEIN Na WACHIRA MWANGI

WAUMINI wa Kanisa la Good News International linalohusishwa na Paul Mackenzie walihamishwa kutoka Malindi kuelekea Shakahola kutumia lori lake, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imefichua.

Ufuchuzi huo uliotokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na DCI, umeweka wazi maelezo tata ya safari ya Mackenzie.

Ufichuzi huu unatoa mwanga kuhusu jinsi Mackenzie alivyokengeuka na kuamua kutoka Malindi na kuelekea katika msitu wa Shakahola, kuwavuta wafuasi wake waliojitolea kutoka Kanisa la Good News International hadi ndani ya jangwa hili la ajabu.

Ripoti za kijasusi zilizokusanywa na wapelelezi katika DCI zimefichua Mackenzie aliwahamisha wafuasi wake kutoka Malindi hadi Shakahola ndani ya lori lake.

Wapelelezi hao walibaini kuwa waumini wa Kanisa la Good News International waliwasiliana na kufahamikiana kupitia vikundi mbalimbali kama vile kupitia jukwaa la WhatsApp huku wale waliokuwa wakielekea Shakahola ‘Kwa Mackenzie’ wakipaswa kwanza kupita kwenye makazi ya Mackenzie eneo la Furunzi huko Malindi.

DCI inasema, wafuasi hao walipofika kanisani, walipokolewa na mtu anayeitwa Benjamin, kisha kusafirishwa hadi Shakahola kwa lori jeupe la usajili KCK689W ambalo DCI inaamini ni la Mackenzie.

Lori hilo lina maandishi ‘Kisha Nikaona’ maneno ambayo yalitumika kama jina la video ya muziki ya Mackenzie.

Waumini wengine walibebwa na tuk-tuk na mwanamume aliyejulikana kama Emmanuel wa Tuk Tuk, kwa maagizo kutoka kwa Mackenzie.

Kulingana na DCI, Mackenzie alikuwa na mpango uliopangwa vyema tangu mwanzo hadi mwisho.

Haya yote yalianza mwaka wa 2020 wakati ulimwengu wote ulikuwa unayumbishwa na janga la Covid-19. Serikali ya Kenya wakati huo ilikuwa imeshauri kuhusu umuhimu wa kudumisha umbali baina ya mtu mmoja hadi mwingine.

Wananchi waliombwa na Wizara ya Afya kupunguza idadi katika maeneo ya mikusanyiko kama vile makanisa na misikiti.

Polisi wanaamini kwamba ni hapo ndipo Mackenzie alipochukua fursa ya kuwasajili wafuasi wake kuelekea Shakahola.

Matokeo ya wachunguzi hao yanabainisha kuwa Mackenzie alianza kwa kutangaza kuuza ardhi ya Shakahola kwa njia ya mdomo, mabango, na kushirikishwa kupitia Kundi la WhatsApp la kanisa hilo ambalo wakati huo liliitwa Times TV Team.

Baadhi ya wafuasi wa Mackenzie walikuwa wamepoteza kazi zao ambazo walizitegemea kama chanzo chao cha mapato huku vita vya kitabibu dhidi ya Covid-19 vikiendelea.

Wadadisi wanaamini kutokana na hali hiyo, Mackenzie alitumia umaarufu wake na kuanza kuuza sehemu za ardhi kwa wafuasi wake ambao sasa walikuwa wakihitaji njia yoyote ya kuishi.

Ekari moja iliuzwa kwao kati ya Sh1,000 na Sh3,000, bei ambayo DCI inaeleza kuwa ya chini isiyoendana na hali ya soko la ardhi.

Wakati mtu alinunua ardhi kutoka kwa Mackenzie hakupewa hati yoyote au risiti ya aina yoyote kama thibitisho la umiliki wa ardhi.

Malipo hayo yalifanywa kwa pesa taslimu au kwa M-Pesa huku wengine wakimtumia moja kwa moja  Mackenzie.

Kwa wengine, malipo hayo yalitumwa kwa wakala wa ardhi wa Mackenzie anayejulikana kama Alex Wa Mashamba almaarufu Alex Wa Bethlehem.

Matokeo ya DCI yanabainisha kuwa Alex alifanya kazi kama mpimaji ardhi wa Mackenzie, ndiye aliyewagawia wafuasi sehemu ya ardhi mara tu malipo yalipokamilika, lakini hapakuwa na makubaliano rasmi ya kuuza ardhi kati yao.

Kulingana na mzee wa kijiji Shakahola, Bw Changawa Mangi, Mackenzie alifika Shakahola pekee yake mwaka wa 2021, mwaka huo huo ukoo wa Wamwabaya Mwaro ndani ya eneo la Shakahola waligundua watu wasiowafahamu ambao wanadai walivamia ardhi ya mababu zao.

Ndipo wazee hao walimwendea Mackenzie ambaye alidai kuwa shamba hilo aliuziwa, jambo ambalo wazee walilibaini kuwa ni uongo lakini baadaye Mackenzie akakubali kuinunua kwa kile kilichojulikana kama KAJAMA kumaanisha ‘kuthaminiwa’ kwa lahaja ya Giriama.

“Katika mkataba wa uuzaji wa ardhi ambao haujatiwa saini wa mwezi Machi tarehe 10, 2021, Mchungaji Paul Mackenzie alilipa malipo ya awali ya Sh800,000. Baadaye, katika mkataba wa uuzaji wa ardhi wa Desemba 11, 2021, mkataba wa uuzaji ulirekebishwa kutoka Sh800,000 kwa ekari 800 hadi Sh500,000 kwa ekari 500,” ripoti ya DCI ilisoma kwa sehemu.

Kufuatia kununuliwa kwake, Mackenzie aliita ardhi hiyo iliyoteuliwa kuwa Vilinge, ambayo iko takriban kilomita 72 kutoka mji wa Malindi, lakini wenyeji waliita Shakahola Kwa Mackenzie.

Mhubiri Paul Mackenzie akijadiliana na wakili Wycliffe Makasembo katika Mahakama ya Shanzu wakati wa kutajwa kwa kesi dhidi yake mnamo Julai 3, 2023. PICHA | KEVIN ODIT

Wafuasi wa Mackenzie walipofika Shakahola, walipokolewa katika hema au nyumba ambayo wakazi wake walikuwa wamesafiri. Mahema yalikuwa mawili, moja ya wanaume na nyingine ya wanawake.

Hapa, wangepiga kambi hadi malipo ya ardhi yatakapokamilika ambapo mtu anaruhusiwa kuweka nyumba yake.

Nyumba zote za Shakahola zilikuwa za matope na paa zake ziliezekwa kwa makuti au nyasi, pamoja na nyumba ya Mackenzie.

  • Tags

You can share this post!

Arati apiga abautani kuhusu tozo za kesha, mikutano ya...

Omanyala atema kocha Ayiemba na kuajiri kocha Kimani

T L