• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Arati apiga abautani kuhusu tozo za kesha, mikutano ya Injili

Arati apiga abautani kuhusu tozo za kesha, mikutano ya Injili

NA WYCLIFFE NYABERI

GAVANA wa Kisii Simba Arati ameamuru kuondolewa kwa kifungu cha Mswada wa Fedha 2023 wa gatuzi hilo, kilichonuia kutoza ushuru maombi ya usiku almaarufu ‘kesha’.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Taifa Leo kuangazia mswada huo ambapo wahubiri wangelipa maelfu ndiposa waruhusiwe kufanya kesha na kuendesha injili mitaani.

Kwenye mswada huo, makanisa ambayo yangefanya maombi ya mkesha wa usiku yangelipa Sh5,000 kila wiki.

Naye mhubiri yeyote ambaye angekanyaga mitaani kueneza Injili, angelazimika kutenga Sh2,000 kwa wiki ili aruhusiwe kuhubiri.

Ada hizo zilikuwa kubwa zaidi kwa wahubiri ambao wangetumia magari ya kubebea mizigo yenye vipaza sauti kwani wangehitajika kulipa hadi Sh20,000 kwa wiki.

Mapendekezo hayo yaliibua hisia kali miongoni mwa washikadau wa makanisa, huku wakimsihi gavana Arati asiutie saini mswada huo ambao tayari ulikuwa umepitishwa katika Bunge la Kaunti.

Viongozi hao wa makanisa hawakusita kunukuu vifungu vya Bibilia kuhusu wafalme kama Nebcadnezer wa Babiloni, aliyejaribu kulikandamiza kanisa lakini ufalme wake ukaporomoka.

Pia waliwakumbusha viongozi wa kisiasa kuhusu walikomalizia aliyekuwa kiongozi mdhalimu Adolf Hitler wa Ujerumani na Benito Mussolini wa Italia kama tahadhari kuhusu sera hizo.

Wakihutubia wanahabari Jumatatu jioni kuhusu hisia zilizoibuliwa na makanisa, madiwani hao walisema gavana Arati aliwaamrisha wafanyie Mswada huo mageuzi kwa kukifuta kifungu hicho cha kutoza kesha ushuru.

“Tumeambiwa mapendekezo ya kutoza ushuru kesha za makanisa yameibua joto kali. Hayo hayakuwa makusudio yetu bali yaliletwa na baadhi ya wananchi wakati wa kukusanya maoni hasa mjini Suneka. Walisema baadhi ya makanisa yalikuwa yakiwasumbua kwa kucheza muziki kwa sauti ya juu. Hivyo tuliona ni vyema kudhibiti hali hiyo lakini kwa kuwa imeleta joto, tozo hizo hazitakuwa,” akasema mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kisii Peter Otachi, ambaye pia ni diwani wa Monyerero.

Bw Otachi alisema kulikuwa na maoni kutoka kwa raia kuzitoza ushuru harusi lakini wakayatupilia mbali kwani hatua hiyo ingewazuia raia wengi hasa vijana kufanya fungate za ndoa.

Licha ya tangazo hilo hata hivyo, Jukwaa la Wachungaji na Wahubiri wa Kisii limesema bado haliamini kuwa tozo hizo hazitatekelezwa.

“Kuongea katika vyombo vya habari hakutoshi. Hatuna uhakika kuwa hawatatekeleza ushuru huo kwa kuwa serikali ina ujanja mwingi wa kufanya mambo. Tunaomba kuitwa na kutia saini makubaliano na viongozi wa kaunti ili kuondoa utata wa suala hilo,” akasema mwenyekiti wa jukwaa hilo Bw Lawrence Nyanuga.

  • Tags

You can share this post!

Ziara 38 ndani ya mwaka mmoja!

Waumini wa kanisa la Good News International walisafirishwa...

T L